Rais John Magufuli leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) kitaifa. Kwa mujibu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), sherehe hizo zitafanyika kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).
Rais Magufuli aliwasili mjini Moshi juzi akitokea mkoani Dodoma na jana alishiriki Ibada za Jumapili katika makanisa mawili tofauti, na leo anatarajiwa kuongoza maelfu ya wakazi wa Moshi na miji jirani katika kilele cha sherehe hizo za Mei Mosi, huku wafanyakazi wakililia hali bora makazini.
Akizungumza wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Tucta, Yahaya Msigwa alisema, “Tayari tumemwandikia Rais Dk Magufuli kumuomba awe mgeni rasmi, kimsingi sherehe zote kitaifa mgeni rasmi ni yeye...tunazo ajenda za kumpa Rais, lakini moja ya mambo ambayo ni kero ni hili la mikataba ya hali bora kazini, wafanyakazi wengi wanafanya kazi kama vibarua na hawajui haki zao.”
Kwa mujibu wa takwimu za Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Taifa lilipaswa kuwa na waajiriwa milioni 3.7 katika sekta iliyo rasmi, lakini waliopo ni 650,000 pekee hali inayoashiria kutokuwa na mikataba.
Alitolea mfano wa watumishi wa mashambani pekee nchini Kenya ni zaidi ya 700,000 na Afrika Kusini ni zaidi ya milioni moja na kwamba ipo haja kwa waajiri Tanzania kutafakari upya suala la maslahi ya wafanyakazi wao na rais anapaswa kulisemea hilo.
Post a Comment