Na Regina Mkonde
Rais John Magufuli Jumamosi ya Mei 20, 2017 katika mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)anatarajiwa kumkabidhi kijiti cha uenyekiti wa jumuiya hiyo Rais wa Uganda, Yoweli Museveni baada ya Tanzania kuingoza EAC kwa vipindi viwili mfululizo.
Hayo yamesemwa jana Mei, 18 na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga katika Mkutano wa 34 wa Baraza la Mawaziri la EAC, ambapo alieleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi ambacho Tanzania iliiongoza jumuiya hiyo, ikiwemo kuridhia maombi ya muda mrefu ya uanachama, ya nchi ya Jamhuri ya Sudan Kusini na kuipatia uanachama kamili wa jumuiya hiyo.
“Tanzania tumemaliza muda wetu baada ya kuiongoza vipindi viwili mfululizo, Rais Magufuli Jumamosi atamkabidhi uenyekiti Rais Museveni wa Uganda,” alisema.
Alieleza kuwa, pamoja na Rais Magufuli kukabidhi kijiti hicho kwa Museveni, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa anatarajiwa pia katika mkutano huo kuwasilisha ripoti ya mazungumzo ya pamoja ya kuleta amani, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la wakuu wa nchi wa EAC lililotolewa mwezi Januari,2017.
Kuhusu mkutano wa Baraza la Mawaziri wa EAC uliofanyika jana Mei 18, 2017, alisema wajumbe wa baraza hilo watajadili ushirikiano wa masuala mbalimbali yanayohusu jumuiya hiyo, ikiwemo ushirikiano kibiashara, uwekezaji, elimu pamoja na huduma mbalimbali za kuendesha nchi wanachama hasa ujenzi wa miundombinu na uchukuzi.
“Kwanza Tanzania itatoa ripoti ya ushirikiano kwa kipindi cha miaka miwili iliyoiongoza EAC ikiwemo ya ushirikiano kibiashara, kielimu na huduma za kuendesha nchi,” alisema.
Alisema wajumbe hao watajadili namna ya kuondoa na au kupunguza vikwazo visivyo vya kisheria hasa vinavyokwamisha biashara ikiwemo ushuru wa forodha, vizuizi vya magari, aina za biashara, na kwamba watajadili namna ya kuanzisha soko imara la pamoja.
“Kuna vikwazo visivyo vya lazima vinavyokwamisha biashara kwa nchi wananchama, mfano Tanzania tuna vyombo viwili vinavyopima ubora wa bidhaa, TBS na TFDA ambapo wenzetu wanasema ngazi hizi mbili zinazuia biashara zao, kwa hiyo tutazungumzia suala hili. Pia tutajadili namna ya kutekeleza lengo letu la kuzuia uingizwaji wa nguo za mitumba kutoka nchi za nje ya jumuiya hii,” alisema.
Kwa upande wa elimu, Balozi Mahiga alisema wajumbe hao watajadili namna ya kuanzisha mfumo wa elimu ambao utasaidia kuondoa tofauti ya upatikanaji elimu katika vyuo vya EAC ikiwemo wanafunzi wa jumuiya hiyo kupata elimu kwa malipo na vigezo vinavyo fanana na kwamba kusiwepo na vikwazo.
“Tulikuwa na chuo kimoja tu cha jumuiya, lakini sasa tuna vyuo tanzu katika nchi ya Tanzania, Kenya na Uganda kwa hiyo kuna umuhimu wa kuwa na mfumo wa elimu kwa wanafunzi kupata elimu kwa malipo na vigezo vinavyofanana. Mwanafunzi wa Tanzania akienda Kenya asome kwa vigezo na gharama ileile anayolipa mwanafunzi wa Kenya,” alisema.
Post a Comment