RAIS John Magufuli amesema serikali inawachunguza watumishi wa umma waliogushi umri ili wasibaki kwenye utumishi wa umma kwa muda ambao hawakustahili kuwa kazini.
Kadhalika, amesema kuna watumishi wenye miaka 60 na zaidi ambao hawataki kustaafu huku waking’ang’ania ajira na madaraka, na wengine wakijipachika vyeo vya ukurugenzi.
Akizungumza katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi) ambazo kitaifa zilifanyika jana katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Rais Magufuli alisema uchunguzi huo wa umri umeshaanza.
“Wako watumishi ambao wamebadilisha umri wao," alisema Rais Magufuli. "Wamebadilisha miaka yao na unakuta ni mzee kabisa, lakini kabadilisha umri.
"Kuna watu ambao ni wazee tena kuliko mimi. Wanasema hawaondoki eti ndio wakati umefika, hao nao tunawachunguza.”
Katika hotuba yake, Rais Magufuli alisisitiza kuwa wapo watumishi wa umma ambao bado wanafanya kazi wakiwa wameshatimiza umri wa kustaafu kwa lazima wa miaka 60 lakini hawataki kustaafu ili kuachia nafasi wegine waajiriwe.
Watoto wa viongozi
Alisema katika watu walioghushi vyeti, kuna baadhi ni watoto wa viongozi ambao walijipatia ajira bila uhalali huku watoto wa maskini wamekuwa hawaendi kokote, licha ya kuwa na vyeti halisi.
Alisema kwa sababu hiyo serikali ilisimamisha ajira kwa muda mrefu, kwa kuwa wafanyakazi walikuwa ni wengi wakiwemo hewa na wenye vyeti vya kughushi.
Rais aliwahoji wafanyakazi, “Hivi mlitaka nipandishe mishahara niwapandishie ndani humo na wale wafanyakazi hewa na watu wa kughushi vyeti, ndio maana nilitaka kwanza nisafishe nyumba.
Alisema kwa sasa mwelekeo ni mzuri na atakapopandisha mshahara atafanya hivyo kwa watumishi sahihi na ndio nia ya serikali.
Alisema wafanyakazi hewa, sio jipu maana halionekani, ila wafanyakazi wenye vyeti feki wapatao 10,000 ndio majipu na ameamua kuwatumbua, maana ndio walikuwepo. Alisema ameshaagiza watu wote ambao wameorodheshwa kwenye orodha ya vyeti feki, wajiondoe ndani ya siku 15.
“Waondoke hata kama ni mtoto wa waziri au wa rais, yeyote anayehusika aondoke. Akigoma apelekwe mahakamani na huko najua kifungo chao sio chini ya miaka saba,” alisema Rais Magufuli.
Hata hivyo, alisema kwamba anachojua, watumishi hao wenye vyeti feki watajiondoa tu wenyewe kwa kuwa mishahara hawataendelea kupata.
Rais Magufuli alisisitiza kuwa viongozi wa juu, hawana nia mbaya kufanya uhakiki huo, bali wana nia nzuri, kwani wanataka watumishi ambao wanadai maslahi yao yaboreshwe, yaende kwa watu sahihi.
Rais Magufuli alisema serikali inataka kila kazi iwe na mfanyakazi mwenye sifa stahiki na kama ni ya darasa la saba, afanye mtu mwenye elimu hiyo na sio kughushi cheti.
Alisema serikali imefanya uhakiki huo ili kama ni mtu wa darasa la saba, aombe kwa sifa ya cheti chake na sio kwenda kufoji cheti cha kwenda kufanya kazi ya uuguzi wakati hajafikia sifa hiyo.
Rais alisema kuna wakurugenzi wa mashirika na taasisi za serikali ambao wameghushi vyeti, halafu wanawanyanyasa watu wa chini ambao hawana vyeti vya kughushi. Alisema watu hao walioghushi, hawastahili nafasi hizo na ndio maana Serikali imeamua kuwaondoa.
Post a Comment