Kada wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Abdallah Safari amemfagilia Rais Magufuli kwa kupigania rasimali za taifa ikiwemo madini yaliyokuwa yakiwanufaisha Wawekezaji.
Akizungumzia hatua ya Rais Magufuli kuitisha tume mbili za uchunguzi wa Mchanga wa Madini na kubaini madudu kwenye uwekezaji katika sekta ya Madini ikiwemo baadhi ya kampuni kutosajiliwa ikiwemo kampuni ya ACACIA, Prof Safari amesema kutokana na juhudi binafsi anazofanya kutetea rasilimali za nchi anamfananisha Magufuli na Rais wa Kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah na Waziri Mkuu wa Kwanza wa Congo (DRC), Patrice Lumumba
Licha ya Prof.Safari mwingine aliyempongeza Rais Magufuli ni Mbunge wa Chambani, Yusuf Salim Hussein (CUF) ambaye amesema anamuunga mkono Rais Magufuli, kwani amejitoa mhanga kwa maslahi ya taifa.
Aliongeza kuwa vita hiyo ni ngumu na wanapaswa kumshukuru Rais bila ya kujali kama ni wa CCM, Chadema au CUF.
“Ninampongeza Rais John Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kutetea rasilimali za nchi. Anafanya kazi kama walivyokuwa wanafanya baadhi ya viongozi wazalendo barani Afrika ya kupigania haki za wananchi wao kufaidika na rasilimali za nchi,” alisema Profesa.
Alitoa mfano wa Patrice Lumumba, Kwame Nkrumah na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kama viongozi waliojitolea kwa ajili ya wananchi wao.
Alisema maamuzi anayoyafanya Rais yanasimama katika Kifungu cha Tisa (Kifungu Kidogo C) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho ya mwaka 2000, ambacho kinasisitiza kwamba utajiri wa Taifa uendelezwe, uhifadhiwe na kutumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine.
Profesa Safari aliwaomba Watanzania na wataalamu wa sheria za mikataba, kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais katika kutetea maslahi ya Taifa.
“Nchi hii ina wanasheria wengi wazuri katika masuala ya madini na mikataba. Ninashauri watafutwe wataalamu hawa watakaokuwa sio wala rushwa ili wamsaidie Rais katika vita hii ya rasilimali,”aliongeza Profesa Safari.
Juzi Rais Magufuli alipokea ripoti ya Kamati ya Pili ya Madini ya kuangalia masuala ya kisheria na kiuchumi, ambapo ilionesha Serikali imekuwa ikipoteza mapato ya Sh trilioni 108.46 kutokana na udanganyifu, unaofanywa katika usafirishaji wa mchanga wa dhahabu ‘makinikia’ nje ya nchi katika kipindi cha kuanzia mwaka 1998 hadi mwezi Machi 2017.
Wakati huo huo, Bunge linatarajiwa kutoa Azimio la kumuunga mkono Rais Magufuli kutokana na kazi nzuri, zilizofanywa na kamati mbili alizoziteua kuchunguza mchanga wa dhahabu (makinikia) zilizobaini wizi mkubwa, anaripoti Mgaya Kingoba kutoka Dodoma.
Wabunge wengi wakiwamo wa Kambi ya Upinzani, walisema jana kuwa wameikubali kazi nzuri inayofanywa na Rais Magufuli katika suala la madini, ingawa wao walinyoosha kidole kwa Serikali ya CCM kuwa ilishindwa kuzuia wizi huo.
Wabunge wote waliochangia jana walitoa pongezi kwa Rais Magufuli kutokana na kazi nzuri ya kamati zake mbili; ya kwanza ya wataalamu wa jiolojia na kemia na ya pili ya wachumi na wanasheria, ambazo zimeibua wizi mkubwa uliofanywa na kampuni za uchimbaji madini.
Post a Comment