Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Zitto Kabwe ametuma salamu za rambi rambi kwa wanachama wa Chadema baada ya kuondokewa na kiongozi wake mkubwa, Philemon Ndesamburo.
Pia Zitto amempa pole, mtoto wa marehemu Ndesamburo, Lucy Owenya kwa kumpoteza baba yake.
Zitto ameandika katika ukurasa wake wa Facebook leo na kusema; “Ni msiba mkubwa kwa watu wa Kilimanjaro na hasa Moshi Mjini ambapo Mzee Ndesa Pesa alikuwa mwakilishi wake Bungeni kuanzia Mwaka 2000 mpaka Mwaka 2015. Kilimanjaro imepoteza mtu ambaye aliweka maslahi ya mkoa wake mbele kuliko kitu kingine chochote.”
Zitto amesema msiba wa Ndesamburo ni mkubwa kwa wanaChadema ambacho alikuwa Mwenyekiti wake wa Mkoa tangu chama kimeanzishwa mpaka mauti yalipomkuta.
“Huwezi kutaja maendeleo ya Chadema kwa nchi yetu bila ya kutaja jina la mzee Ndesamburo. Nimepata bahati ya kufanya naye kazi kwa karibu, naweza kutamka bila wasiwasi kwamba ni mmoja wa watu waliokipenda chama chake kwa dhati kabisa,” amesema
Kadhalika Zitto anaendelea kummwagia sifa Ndesamburo akisema Tanzania ina faidi matunda ya vyama vingi kwa sababu ya kazi kubwa aliyofanya Mzee Ndesamburo.
“Nawapa pole Sana watoto, wajukuu na vitukuu vya Mzee Ndesamburo. Mzee wetu aliishi maisha yake na ameacha ' legacy ' yake. Najua maumivu yenu lakini tupo wengi tunaoumia nanyi. Mungu awavushe kwenye mtihani huu mkubwa. muwe wamoja na mshikamane.” Amesema na kuongeza:
“Poleni sana ndugu zangu wa Chadema kwa kupotelewa na kiongozi wenu na kiongozi wetu pia. Poleni sana wana Moshi Mjini na wana Kilimanjaro wote. Poleni Sana Watanzania.pumzika kwa Amani Philemon Kiwelu Ndesamburo. Hiyo ni njia yetu sote. Amina.”
Post a Comment