Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Vigogo watatu Chadema motoni

WAKATI Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Dk. Vicent Mashinji, akipelekwa mahabusu mkoani Ruvuma na Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho, Tundu Lissu, akigoma kutoka mahakamani kwa hofu ya kukamatwa Dodoma,-

kigogo mwingine wa Chadema, Edward Lowassa, naye anatarajiwa kukiona cha moto leo jijini Dar es Salaam.

Dk. Mashinji na viongozi wengine wanane wa Chadema, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Ruvuma kujibu mashitaka mawili kabla ya kunyimwa dhamana na kupelekwa mahabusu.

Viongozi hao walifikishwa mahakamani hapo jana saa 3:45 asubuhi na kusomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Renatus Mkude ambaye alikuwa akisaidiwa na Wakili wa Serikali, Shaban Mwigole mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Simon Kobelo.

Mjini Dodoma, Lissu aligoma kutoka ndani ya Mahakama ya Wilaya ya Dodoma baada ya kupata taarifa kuwa anatakiwa kukamatwa na Polisi na kupelekwa Dar es Salaam.

Tukio hilo lilitokea jana Mahakamani hapo baada ya kuahirishwa kesi ya Chama cha Walimu (CWT) Manispaa ya Dodoma, iliyokuwa inahusu mgogoro wa viongozi wa chama hicho.

Katika kesi hiyo, Lissu alikuwa wakili wa utetezi wa viongozi wapya wa chama hicho wanaodaiwa kufanya matumizi mabaya ya mali za CWT.

Nipashe ilishuhudia polisi waliokuwa wamevaa kiraia huku gari lao likiwa limeegeshwa jirani na lango la kuingilia viwanja vya Mahakama Kuu ya Dodoma.

Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo ambayo ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Proches Mushi, hadi Septemba 27, Lissu aliiambia mahakama kuwa amepata taarifa kwa njia ya ujumbe mfupi kuwa akitoka mahakamani hapo atakamatwa, hivyo atakuwa mfungwa.

Lissu alisema amepata taarifa za kutaka kukamatwa kupitia ujumbe mfupi aliotumiwa na mkewe toka Dar es Salaam na asubuhi askari walifika nyumbani kwake na kujulishwa kuwa yuko Dodoma.

“Sitatoka mahakamani hapa," alisema Lissu. "Kama wao wana uwezo na wanafanya kazi kwa maelekezo waje wanikamatie hapa mahakamani."

"Sitoki, nitaendelea kunywa maji yangu haya yatanipa nguvu ya kukaa hadi jioni.”

Hata hivyo, alipoulizwa na Nipashe, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, alisema hawana mpango wa kumkamata na kwamba wakitaka kumkamata hata ndani ya mahakama wana uwezo huo.

“Kama anaogopa polisi kwa nini anazungumza maneno yasiyofaa mbele ya jamii?” alihoji Mambosasa.

Jijini Da es Salaam, Waziri Mkuu mstaafu, Lowassa huenda naye akafunguliwa mashitaka ya uchochezi mahakamani leo kama kauli ya Lissu ya mwanzoni mwa wiki ni ya ukweli.

Lowassa anatakiwa kuripoti kwa mara ya nne Makao Makuu ya Jeshi la Polisi ambako Lissu alidai alipata taarifa kuwa atakamatwa na kupelekwa mahakamani.

Lowassa ambaye aliwania urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika Uchuguzi Mkuu wa mwaka 2015, anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi jijini wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema).

Katika hafla hiyo, Lowassa alimtaka Rais John Magufuli kutafakari upya hatima ya masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumuki), maarufu Uamsho, wanaoshikiliwa mahabusu kwa zaidi ya miaka minne wakikabiliwa na mashitaka ya ugaidi.

Alisema ni jambo la fedheha kwa nchi iliyopata uhuru zaidi ya miaka 50 kuwaweka mahabusu viongozi wa dini bila kesi kusikilizwa mahakamani.

Kutokana na matamshi hayo, DCI alimwandikia barua ya kumhitaji kwa mahojiano.

Mjini Songea, Mkude alidai mahakamani hapo kuwa washitakiwa wote kwa pamoja wanashitakiwa kwa makosa mawili ambapo kosa la kwanza, wote kwa pamoja, wakiwa Wilayani Nyasa tarehe isiyofahamika, walikula njama ya kutenda kosa ambalo lingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Alidai kosa la pili, Julai 15, mwaka huu katika eneo la mji wa Mbambabay, washitakiwa wote kwa pamoja walifanya mkusanyiko usio wa halali uliokuwa unapelekea uvunjifu wa amani kwa jamii.

Aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa. Washitakiwa wote wamekana mashitaka yote mawili.

Ingawa dhamana yao iko wazi, washtakiwa walirudi rumande kwa kuwa Hakimu Kobelo alikuwa amekwenda Mahakama Kuu, Kanda ya Songea na kushindwa kurudi ofisini mpaka saa za kazi zilipomalizika.

Wakili wa Serikali Mkude aliwataja washitakiwa wengine kuwa ni Cecil Mwambe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini na Mbunge wa Jimbo la Ndanda mkoani Mtwara, Philberth Ngatunga (Katibu Kanda ya Kusini), Irineus Ngwatura (Mwenyekiti Mkoa wa Ruvuma) na Delphin Gazia (Katibu wa Mkoa wa Ruvuma).

Wengine ni Zubeda Sakuru (Mbunge wa viti maalum Ruvuma), Sanguru Manawa (Katibu wa Oganaizesheni na Mafunzo), Curthberth Ngwata (Mwenyekiti wilaya ya Nyasa ambaye pia ni Diwani wa kata ya Kipingu) na Chalres Makunguru (Katibu mwenezi wilaya ya Nyasa).

*Imeandikwa na Renatha Msungu, DODOMA, Gideon Mwakanosya, SONGEA na Gwamaka Alipipi
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top