Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki, Mb (kulia) akiwasili katika Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni leo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Wilaya hiyo kuzungumza na Watumishi wa Umma. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Ally S. Happi akimkaribisha Waziri Kairuki, na kushoto ni Mkurugenzi wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Aron Kagurumjuli
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Ally S. Happi akizungumza na watumishi wa umma wa wilaya ya Kinondoni leo (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) katika Wilaya hiyo kuzungumza na Watumishi wa Umma, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Kinondoni (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi katika wilaya hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni Bibi. Sixtha Kevin Komba akiwasilisha hoja wakati wa kikao kazi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) alipofanya ziara ya kikazi katika wilaya ya Kinondoni leo Jijini Dar es Salaam.
Afisa Utumishi Mwandamizi kutoka Idara ya Ukuzaji Maadili Ofisi ya Rais- Utumishi Bi. Leyla Mavika akitoa ufafanuzi kuhusu masuala ya maadili katika Utumishi wa Umma wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) katika Wilaya ya Kinondoni leo Jijini Dar es Salaam.
Mstahiki Meya Manispaa ya Kinondoni Mhe. Benjamini Sitta (kulia) akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) baada ya kupokea hoja za watumishi wa Umma wa Wilaya ya Kinondoni leo Jijini Dar es Salaam. Pichani- Katikati ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) na kushoto ni Mkurugenzi Manispaa ya Kinondoni Bw. Aron Kagurumjuli. Picha na: Genofeva Matemu - MAELEZO
Waajiri nchini wametakiwa kufanya uhakiki wa kina wa vyeti vya elimu kwa ajira mpya zitakazotolewa ili kuwa na watumishi wa umma wenye sifa zinazostahili katika utumishi wa umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) amesema hayo leo katika kikao kazi na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Kairuki amesema uhakiki wa kina utasaidia sana kuepukana na kutojirudia tena kwa suala la watumishi wa umma wanaoghushi vyeti.
“Jana tumetoa vibali vya ajira 10,184 kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekretarieti za Mikoa, Wakala za Serikali, pamoja na Taasisi na Mashirika ya Umma ili kujaza nafasi zilizoachwa na watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti vya elimu, hivyo napenda niwasisitize sana waajiri wote kufanya uhakiki wa kina ili tusiwe tena na watumishi wa umma wasiostahili katika orodha ya malipo” Mhe. Kairuki amesema.
Waziri Kairuki amesisitiza kuwa zoezi la uhakiki ni endelevu ambapo lazima lifanyika pale mtumishi wa umma atakaporudi katika kituo cha kazi kutoka masomoni, na watakaorejea katika utumishi wa umma baada ya likizo bila malipo au sababu nyingine.
“Tunafanya hivi sio kwa nia mbaya, bali tunataka tuwe na watumishi wanaostahili kuwepo katika utumishi wa umma kwa sababu wanaoghushi wanaziba nafasi za wale wanaostahili kuwepo na wenye sifa katika utumishi wa umma” Mhe. Kairuki aliongeza
Pia amewataka Waajiri kusafisha taarifa wa watumishi wa umma mara kwa mara katika Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS).
“Kuna watumishi ambao muda wao wa kuwepo kazini umemalizika (wamestaafu) lakini bado wanaendelea kuwepo, Mfumo wa HCMIS sasa kila ifikapo saa 06:01 usiku utakuwa unawaondoa wale wote ambao muda wao wa kuwepo kazini umefika lakini bado wanaendelea kuwepo kwenye Mfumo.
Mhe, Kairuki yuko katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Dar es Salaam, ambapo leo ni siku yake ya nne aliyoitumia kukutana na Watendaji na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, baada ya kuzungumza na watumishi wa umma wa Temeke na Mbagala.
Lengo la ziara ni kukutana na watumishi wa umma na kusikiliza malalamiko, ushauri na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kuzifanyia kazi na kuleta mabadiliko katika Utumishi wa Umma nchini.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Rais-UTUMISHI
13.07.2017
Post a Comment