Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imegoma kupokea bangi inayodaiwa kukutwa nyumbani kwa Mlimbwende Wema Sepetu, kama kielelezo.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ametoa uamuzi huo leo Agosti 31, kutokana na hoja za kupinga kupokelewa zilizowasilishwa na Wakili wa Wema, Tundu Lissu.
Awali Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Mkemia kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Elias Mulima akiongozwa na Wakili wa Serikali, Costantine Kakula aliomba kutoa bangi kama kielelezo katika kesi hiyo mahakamani ambayo alidai kupima msokoto mmoja na vipisi viwili vinavyodaiwa kukutwa nyumbani kwa Wema na kugundua ni bangi.
Mulima aliomba kuitoa bahasha iliyofungwa, yenye muhuri, saini ya shahidi huyo na namba ya maabara 291 ya 2017 mahakamani hapo kwa utambuzi.
Wakili Lissu alipinga kisipokelewe kama kielelezo cha ushahidi kwa sababu ndani ya bahasha hiyo kuna vitu zaidi ya msokoto mmoja na vipisi viwili vinavyodaiwa kuwa ni bangi.
“Mheshimiwa hakimu vipisi viwili vyenye majani ukiviangalia kwa makini ni vishungi vya sigara ambayo imetumika kwa sababu vina alama ya kuungua, kwetu vinaitwa twagooso, kitu kinachoitwa msokoto wa bangi hakijulikani kimefungwa fungwa tu karatasi, kuna kibiriti, karatasi nyekundu, haiwezekani vitu vilivyotolewa kwenye bahasha kuwa ndiyo vitu shahidi alivielezea, mahakama isikubali kuvipokea kama kielelezo,”alidai Lissu.
Baada ya mahakama kugoma kupokea kielelezo hicho imepanga kuendelea kusikiliza ushahidi wa Jamhuri Septemba 12 na 13 mwaka huu. Wema na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia dawa za kulevya.
Post a Comment