MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Itebulanda wilayani Urambo Mkoa wa Tabora, George Nicholaus, amehukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh. milioni moja baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili.
Hukumu hiyo, ilitolewa na hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Hassan Momba, baada ya mwalimu huyo kukiri makosa ya ufujaji, ubadhirifu na kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu akiwa mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo.
Mwalimu huyo alifikishwa mahakamani Julai 28 mwaka huu na baada ya kusomewa mashtaka hayo mawili alikana, Ijumaa shauri hilo, lilipoitishwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali bila kushurutishwa, alikiri kutenda makosa hayo.
Hakimu Momba alitoa uamzi wa shauri hilo, kuwa kwa vile mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na anajutia kosa hilo, mahakama inamhukumu kwenda jela miaka mitatu ama kulipa faini ya Sh. milioni moja.
Awali upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edson Mapalala, uliiambia mahakama kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo kati ya Agosti 2014 hadi Machi 2015 alipokuwa akikaimu nafasi ya mtendaji wa kijiji cha Itebulanda.
Mapalala alidai katika kipindi hicho, mshtakiwa akiwa ni mwajiriwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kama mwalimu mkuu na kaimu ofisa mtendaji wa kijiji cha Itebulanda alifuja Sh. 1,701,000, mali ya mwajiri wake.
Mapalala aliongeza kudai mwalimu huyo, alitenda kosa la ufujaji wa kiasi hicho cha fedha kwa kuwa zilikuwa chini ya umiliki wake.
Loading...
Post a Comment