Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imekataa kuiongezea muda wa leseni Kampuni ya Kufua Umeme wa Independent Power Tanzania Limited (IPTL) baada ya leseni yake ya kuzalisha umeme kumalizika muda wake.
Kwa mujibu wa tangazo la Ewura, lililotolewa kama taarifa kwa vyombo vya habari , maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa Ewura kilichofanyika Agosti 30, mwaka huu.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Machi 28, mwaka huu, Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) iliwasilisha kwa Ewura maombi ya kuongeza muda wa leseni ya kuzalisha umeme kwa miezi 55 kuanzia Julai 16, 2017 hadi Januari 15, 2022.
“Bodi ya Wakurugenzi ya Ewura katika kikao chake kilichofanyika tarehe 30 Agosti 2017, imefikia uamuzi wa kukataa maombi ya kampuni ya IPTL baada ya kuzingatia mambo yafuatayo,” ilieleza taarifa hiyo ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura.
Iliyataja mambo yaliyozingatiwa na bodi hiyo kuwa ni athari hasi kwenye bei ya umeme kwa watumiaji endapo muda wa leseni ya IPTL ungeongezwa ikiwa ni pamoja na kuendelea kulipa malipo ya ‘capacity charge’ kwa kiasi cha dola 2.667 milioni kwa mwezi; pingamizi kutoka kwa umma na wadau mbalimbali; na migogoro na kesi mbalimbali za kisheria zinazoendelea zikiihusisha Kampuni ya IPTL.
IPTL ilikuwa na mkataba wa miaka 20 ambao ulimalizika Julai 16, mwaka huu, na kwa miaka yote hiyo imekuwa ikiiuzia umeme serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kutumia mitambo hiyo ya kufua umeme iliyoko eneo la Salasala Tegeta jijini Dar es Salaam.
Lakini katika miaka ya karibuni, kampuni hiyo imejikuta katika mzozo na wamiliki wake, serikali, umma kwa upande mwingine kutokana na kuonekana ‘kuinyonya’ nchi katika malipo hayo ya umeme ambao unaonekana kuuzwa kwa bei ya juu kuliko uhalisi wake hasa suala la ‘capacity charge.’ Aidha, kumekuwapo na kesi zinazoendelea mahakamani kuhusu umiliki wa kampuni hiyo baada ya kuuziana hisa.
Pia hivi karibuni waliokuwa wabia katika IPTL, Harbinder Singh wa Kampuni ya PAP na James Rugemalira wa VIP Engineering Limited wako mahakamani wakishitakiwa kwa uhujumu wa uchumi na kutakatisha fedha.
Post a Comment