Huku akitia huruma, baadhi ya wananchi jijini hapa wameibua gumzo kuhusiana na nguo anazovaa mfanyabiashara maarufu, Yusufu Manji ambaye ana kesi mbili zinazomkabili.
Manji ambaye alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Februari 17, mwaka huu amekuwa akikabiliwa na kesi mbili, moja ikihusu uhujumu uchumi na ya pili ni madai ya matumizi ya dawa za kulevya.
Baadhi ya wananchi wamekuwa wakidai kwamba wamekuwa wakimshuhudia Manji akija mahakamani akiwa amevaa tisheti ya rangi nyeusi kwa zaidi ya mara kumi, jambo ambalo limeleta gumzo kwa kuwa wanaamini ana nguo nyingi.
“Hatujui sababu, huyu bwana ni tajiri sana lakini kila akifika mahakamani anavaa tisheti nyeusi ileile, kwa nini?” alihoji mwananchi mmoja. Wapo waliomuonea huruma na kudai kwamba inawezekana anafanyiwa figisufigisu kwa kutoruhusiwa kupelekewa nguo na wengine wanadai kwamba inawezekana ameamua mwenyewe awe hivyo kama alivyoamua kutonyoa ndevu.
UWAZI liliamua kumtafuta mtaalamu wa utabiri (Astrologer), Maalim Hassan Yahya Hussein na kumuuliza kuhusu gumzo hilo na amesema nguo hiyo nyeusi anayovaa mfanyabishara huyo ina maana kubwa.
Akizungumza na gazeti hili, Maalim Hussein alisema nguo nyeusi kinyota ina maana nyingi kama vile kuonesha huzuni, msiba, au kupatwa na mkosi. Maalim Hassan aliongeza kuwa inaweza kuwa ni kwa sababu hizo alizozitaja kwamba mshitakiwa anajua kwamba huu ni wakati wake wa huzuni.
“Ni kwamba Manji anajua kuwa yupo shimoni, hivyo anatakiwa afanye kila linalowezekana ili kujinasua, na ndiyo maana ameweka mawakili ili wamnasue kule shimoni,” alisema Maalim Hassan.
Akifafanua zaidi mtabiri huyo alisema nguo nyeusi huonesha pia kwamba ni siku ya mikosi ambayo kinyota ni Jumamosi.
“
Hivyo mtu kuvaa nguo nyeusi iwe ni shati, suruali, jinzi au soksi, inamaanisha ana huzuni na ndiyo maana watu wengine wakifiwa huvaa nguo za rangi hiyo na kwa wale wenye imani nyingine huona kuwa nguo za rangi hiyo huashiria mkosi, hivyo huwa hawazivai hata kama ni siku ya msiba,” alisema.
“Kwa hiyo Manji kuvaa tisheti nyeusi au viatu vyeusi na soksi nyeusi au jinzi nyeusi siyo kwamba hana nguo au viatu vya kubadilisha lakini haina maana kwake kuvaa makoti makubwa ya rangi nyingine kwa sababu ana matatizo, ana huzuni na ni kama yupo shimoni kinyota,” alifafanua mnajimu huyo. Akaongeza:
“Amini kwamba Manji ataendelea kuvaa hivyo mpaka kesi zake zitakapokwisha na licha ya nguo nyeusi hata ndevu zake nyeusi kaziachia, hazinyoi, sababu ni hiyohiyo siyo kwamba hana fedha za kununua wembe wa kunyolea.” Manji hivi sasa ana kesi mbili mahakamani, moja ni tuhuma ya kuhujumu uchumi na ya pili inahusu madai ya kutumia madawa ya kulevya aina ya heroine.
Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha ambaye anasikiliza kesi ya madawa, wiki iliyopita alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi watatu wa upande wa mashtaka
ameridhika kuwa mshtakiwa huyo ana kesi ya kujibu hivyo ana haki ya kujitetea na kuita mashahidi. Wakili wa Manji, Hudson Ndusyepo alidai kuwa mteja wake atajitetea kwa njia ya kiapo na wana mashahidi 15.
Pia aliomba hati ya wito (samansi) kwa ajili ya kuwaita mashahidi hao. Kesi imeahirishwa hadi kesho Agosti, 30 na 31,2017 ambapo Manji ametakiwa aanze kujitetea. Awali upande wa mashtaka ulisema ungeita mashahidi wasiozidi 10 kutoa ushahidi lakini watatu ndiyo waliotoa ushahidi kwenye kesi hiyo.
Manji alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 16, 2017 akidaiwa kuwa kati ya Februari 6 na 9, 2017 katika eneo la Upanga Sea View Ilala alitumia dawa za kulevya aina ya heroine.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Manji alikana kuwa siyo kweli na kwenye kesi hiyo anawakilishwa na Mawakili Alex Mgongolwa, Hudson Ndusyepo na Mosses Kimaro ambapo alipata dhamana baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ambaye alisaini bondi ya Sh. milioni 10.
Hata hivyo, mfanyabiashara huyo, licha ya kupata dhamana katika kesi ya kwanza, yupo rumande kutokana na kesi ya uhujumu uchumi ambapo anadaiwa alikutwa na vitambaa vya jeshi la wananchi na mihuri ya makamanda wa jeshi hilo la lile la kujenga taifa.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilipoketi Agosti 25, mwaka huu iliutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo ili matokeo ya kesi hiyo yajulikane mapema. Rai hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya Wakili wa Serikali, Wankyo Simon kueleza upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na wataeleza hatua ulipofikia katika tarehe itakayopangwa tena.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba aliutaka upande wa mashtaka kuhakikisha wanajitahidi kukamilisha upelelezi ili matokeo yake yajulikane mapema ambapo aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 31, 2017.
Mbali ya Manji, washtakiwa wengine ni Deogratius Kisinda, Abdallah Sangey na Thobias Fwere ambao wanakabiliwa na mashtaka saba chini ya sheria ya Uhujumu Uchumi na Usalama wa Taifa kwa kukutwa na vitambaa vinavyotengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania vyenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 200 na mihuri.
Loading...
Post a Comment