Loading...
Shaka aja kivingine na uchumi kwa Vijana
*HOTUBA YA KAIMU KATIBU MKUU WA UMOJA WA VIJANA WA CCM NDG. SHAKA HAMDU SHAKA (MNEC) ALIYOITOA KATIKA UZINDUZI WA PROGRAMU YA USHIRIKI NA USHIRIKISHWAJI WA FURSA KWA VIJANA KIUCHUMI NA KIJAMII ALKHAMIS TAREHE 7/09/2017 UKUMBI WA WHITE HOUSE - DODOMA*
Ndugu Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma
Ndugu Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini
Ndugu Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dodoma.
Ndugu Waalikwa kutoka makundi mbali mbali
Wawezeshaji wa Programu hii kwa Vijana wa CCM Mkoa wa Dodoma na Washiriki wote.
Kidumu Chama Cha Mapinduzi.
Nachuku fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na uzima na kuweza kukutana muda huu. Pili niwashukuru kwa uamuzi wenu wa kunialika mimi leo kuja kujumuika nanyi nikiwa Mgeni Rasmi katika tukio hili adhimu na muhimu kwa Vijana wa Dodoma; Ahsanteni na mbarikiwe sana. Nasema
Nitumie nafasi hii pia kuwashukuru na kuwapongeza Vijana wote kwa kujitokeza kwenu kwa wingi katika kushiriki uzinduzi wa programu hii muhimu kwa maslahi ya Chama Cha Mapinduzi na Umoja wa Vijana wa CCM.
Kadhalika niwapongeze Viongozi wa UVCCM na CCM Mkoa wa Dodoma kwa kuibua fikra na mawazo ya kuwa na Programu hii ya kuwahamasisha, kuzitambua fursa, Ushiriki na ushirikishwaji Vijana katika miradi ya maendeleo Kiuchumi na Kijamii.
Ndugu Vijana wenzangu.
Mkusanyiko huu umekuwa na Baraka kubwa leo hii kwani ivi karibuni niliongea na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ambaye alinitaka na kuniagiza nitoe Salamu zake kwa Vijana naomba kuwawasilishia salamu hizo kama ifuatavyo:-
Nanukuu
“Nakupongeza Katibu Mkuu kwa juhudi zako za kuendelea kuimarisha Jumuiya yetu ya Vijana ukienda kwenye kikao waambie Vijana mimi nawapenda sana Vijana, niko pamoja nao, wafanye kazi na wawe wazalendo kwa taifa letu.
Natambua mnaendelea na chaguzi katika ngazi mbali mbali waambie wachague Viongozi wazuri, waadilifu, watiifu, wachapa kazi na watakaolinda maslahi ya UVCCM na CCM na sio ya mtu binafsi. Wakatae na wapige vita rushwa kwa nguvu zote na kwa atakaye bainika kutoa au kupokea vyombo vinavyohusika TAKUKURU hatua zichukuliwe haraka” mwisho wa kunukuu maneno ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. John Pombe Joseph Magufuli.
Ni matumaini yangu ujumbe huu mzito kwetu tumepokea, wito wangu kwenu tuendelee kumwombea kwa Mwenyezi Mungu kwa Sala na maombi kila mmoja kwa dini yake Rais wetu. Tumebahatika kupata Kiongozi ambaye muda wote anaonekana kuguswa na kuwa na uchungu na watu wake anaowaongoza akitanguliza mbele na kusisitiza uzalendo kwa Taifa muda wote.
Ndugu Vijana wenzangu
Wazo hili nasema limeibuliwa wakati muafaka huku Serikali ya CCM ya awamu ya tano chini ya Mwenyekiti wa CCM Rais John Pombe Magufuli, ikiweka mkazo na vipaumbele kadhaa vinavyomtaka kila Mtanzania hasa kijana kujituma, kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha mali.
Dhana ya kufanya kazi kwa bidii, malengo na shabaha si ngeni au mpya ila kwa wakati huu inahubiriwa kwa nguvu kulingana na changamoto nyingi zilizopo, fursa, ushiriki na ushirikishwaji pia kwa kuzingatia mahitaji halisi kutokana na mabadiliko ya dunia kiuchumi na kimaendeleo.
Kila mmoja wetu hususan sisi Vijana kwa wakati huu tunahitaji kutambua wajibu wa kukuza shughuli zetu za kazi na maisha zikiongozwa na nguvu ya uzalendo, kujali utaifa na kutambua dhamana iliopo ya kudumisha Amani, Umoja, mshikamano na Maendeleo.
Ili kuishi na kuyajua yote hayo hatimaye vijana waweze kuyafanikisha tunapaswa kuwa na mioyo isiyopwaya au kukosa rutuba ya kutodumisha uzalendo. Tunalazimika kwa pamoja kutambua mpango wowote wa kuyafikia maendeleo ya kweli utabaki ni hadithi na ndoto ikiwa hatutaongozwa na shime ya uzalendo au kutothamini utaifa wetu, kama ambavyo Viongozi wetu wanatuhimiza siku hadi siku.
Ndugu Viongozi na Washiriki wa programu
Pamoja na kuwepo juhudi kubwa za mara kwa mara zinachukuliwa na Serikali, mashirika hiari ya kijamii na yasiokuwa ya kiserikali, kuelimisha juu ya dhana ya ushirikishwaji na ushiriki wa Vijana katika miradi ya kiuchumi na kijamii, tuelewe bila sisi weyewe kuwa na utayari, uthubutu, uzalendo na utaifa, juhudi hizo zitabaki zikielea kama puto juu ya mto au bahari.
Tunalazimika wote kujua kuwa Umoja wa kitaifa na shime ya kukuza uzalendo kwa vijana iwe ni ya pamoja na kila kijana akubali kujadiliana na wenzake juu ya mpango mzima wa maendeleo na hatma ya Taifa na mustakabali wake.
Tufahamu maendeleo kwenye mataifa yalioendelea yametokana na watu wake kukubali kufanya kazi kwani ndiko kulikoyabadili mataifa hayo yaliyoendelea yatoke mahali yalipokuwa katika uchumi duni na kuja katika Uchumi wa Kati na sasa wakionekana kuwa na Uchumi wa Maendeleo ya Viwanda.
Mafanikio hayatakuja kama zawadi kwenye kisahani cha chai au yatokee kwa bahati kama mtende unavyoota jangwani. Wenzetu walikubali kufanya kazi ili kupambana na adui umasikini hatimaye Vijana kwa miguu yao wenyewe wakasimama na kujitegemea kiuchumi na kijamii
Wakati huu ambao Serikali imebeba mzigo wa kutoa elimu bure toka msingi hadi Sekondari ni lazima Vijana tuwe na muktadha mmoja wa kujenga mtazamo wa pamoja kwa kujitambua na kukubali kufanya kazi bila kusukumwa.
Tufahamu kuwa sisi Vijana ndiyo wenye wajibu wa mwanzo wa kuliletea maendeleo Taifa letu kiuchumi au kijamii. Siku zote shughuli za maendeleo ni mzigo wa ushirikishwaji unaokusanya mambo anuai ikiwemo uwezo binafsi wa mtu, kitaaluma, uzoefu, stadi za maisha, kubadilishana fikra juu ya masuala mazima ya aidha mtu kujituma peke yake au kwa kushirikiana na wenzake (kujiunga vikundi).
Ndugu Vijana wenzangu
Nitoe rai na kuwakumbusha kuwa Kazi yetu Vijana siku zote na kila wakati iwe ni kufikiri, kupambanua, kubuni na kujadiliana ili kumalizia changamoto, vikwazo, fursa na matumizi ya nafasi husika katika jamii iliyotuzunguka kwa ajili ya kupeana msukumo utakaoleta tija au kupata faida ya pamoja.
Ndugu Viongozi na Washiriki
Wakati tukizindua programu hii ya Vijana Mkoani Dodoma kwa ajili ya fursa, miradi na ushirikishwaji wa vijana, nadhani yatupasa kufanya hata utafiti mdogo kubaini kwa nini tumekuwa tukirudi nyuma badala ya kwenda mbele. Kwa maoni yangu nadhani kuna mahali tunajikwaa majibu ya utafiti huo utasaidia sana katika kupata njia muafaka za utatuzi.
Kwa bahati nzuri program hii tunaizindua wakati huu chini ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano ambayo inatekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM iliyobeba maudhui makubwa ya kuwasaidia vijana kujikomboa toka katika dimbwi la umasikini. Mkazo mkubwa umewekwa katika kuhakikisha vipaumbele vya ajira kwa vijana vinatekelezeka katika maeneo yafuatayo;
· Uwekezaji na ujenzi wa Tanzania ya Viwanda
· Mifuko ya vijana kupitia ofisi ya Waziri Mkuu na Halmshauri za wilaya.
· Mifuko ya Viongozi wa kisiasa majimboni.
· Elimu ya ujasiriamali na stadi za maisha na maeneo mengine ambayo yameanza kuleta mafanikio.
Kwa fursa ambazo Serikali inazisimamia kupitia ilani ya Uchaguzi ya CCM Sisi vijana tuwe wa kwanza kuzitambua na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake huku tukitumia maarifa yetu katika kufanya kazi za uzalishaji mali na si kushinda mitaani na vijiweni.
Kila Mtanzania anakiri kuwa Nchi yetu ina fursa nyingi, tunayo ardhi kubwa yenye rutuba kwa ajili ya kilimo cha aina mbali mbali, Ufugaji, kazi za ufundi au uendelezaji miradi na ujasirimali. Kwa mshangao baadhi ya vijana wenzetu wanakataa kufanya kazi hizo, je tumejiuliza kwa nini tunatakataa kufanya kazi hizo na je zipi ni kazi mbadala kwetu?
Tunapozumgumzia matumizi ya fursa, kupigania tushirikishwe na ushiriki wetu kama vijana katika miradi ya kiuchumi na kijamii, tuelewa mapema nje ya kazi hizo, Vijana tusitegemee wote kama siku moja tutapata kazi katika sekta ya umma na kukataa kuitumia sekta binafsi/ujiajiri.
Wote hapa tunaelewa mataifa yote yalioendelea vijana wake wamekataa tabia ya utegemezi na kuchagua kazi zipi za kufanya na za kutofanya hatimaye wakajikuta wakipata mafanikio makubwa kiuchumi, kijamii na kuishi kwa kujitegemea.
Hata hivyo uzoefu unaonyesha kuwa kazi zote zinazolinda utu wa mtu, heshima na kumtambulisha thamani yake kama binadamu ni kazi inayostahili kufanywa ili kumpatia mtu kipato halali na kuishi bila kuwa omba omba au mpiga porojo usioyechoka kuzilaumu serikali na kufikiri atakaa bila kufanya kazi na kuamka ukiwa umetajirika.
Ndugu Vijana wenzangu na washiriki wa program
Kabla kumalizia maelezo yangu naomba kuwakumbusha tena kuwa wakati umefika kwa vijana sote nchini kubadilika kifikira na kimtazamo ili tufanye kazi kwa bidii na kujituma. Naomba tuchukue ujumbe huu na kila mmoja kuwa balozi kwa mwezake Taifa letu litajengwa na sisi vijana kwa vile ndio wenye nguvu maarifa, upeo na wenye wajibu wa kufanya hivyo tuache utamaduni wa kulaumu, kulalamika na kukata tamaa badala yake tuwe na tabia ya uthubutu, utayari na kujituma kwa akili na maarifa ili kufanikiwa katika mipango ya kimaisha.
Wazee wetu walifanya kazi nzuri sana ya kupigania Uhuru tumejitawala na sasa tuko huru kazi na jukumu letu sisi vijana sasa ni kujenga uchumi wa nchi, kulinda Uhuru wetu, kuthamini uzalendo na utaifa wetu.
Nduzangu Vijana, Mwisho kabisa nichukue fursa hii kwa mara nyingine tena kuwashukuru na kuwapongeza sana uongozi Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Mkoa wa Dodoma, Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dodoma, watendaji wa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) na wadau wote amabao leo wamefanikisha program hii iweze kukamilika na kuizindua hapa Dodoma.
Hili ni jambo kubwa sana na likifanikwa litakuwa ni chachu na vuguvugu kwa vijana wa Tanzania bila kujali itikadi zao za kisiasa. Kazi ya UVCCM siku zote ni kuonyesha njia za mafaniko hakika vijana wa mkoa wa Dodoma mumetimiza jukumu lenu na kuonyesha kwa vitendo jinsi mnavyomuunga mkono Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli.
Hivyo kupitia mkusanyiko huu nawagiza na kuwataka Makatibu wote Umoja wa Vijana wa CCM wa Mikoa na wilaya nchini kila mmoja kuhakikisha progam hii inaanzishwa katika mikoa na wilaya zao na tunahitaji kuona matokeo yake, tutandaa utaratibu wa kutathimini program hii kila kipindi cha robo.
Mwisho kabisa nawashukuru kwa mara nyingine tena kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika tukio hili la kihistoria mumenipa heshima kubwa nawashkuru na mbarikiwe sana.
Ndugu Vijana wezangu
Baada ya maelezo hayo nitamke Programu hii ya kuwahamasisha, kuzitambua fursa, Ushiriki na ushirikishwaji Vijana katika miradi ya maendeleo Kiuchumi na Kijamii nimeizindua rasmi na sasa sio Dodoma tu ni kwa Vijana wa Tanzania, wahenga walisema Kizuri kula na wenzako.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Kidumu Chama Cha Mapinduzi.
Post a Comment