Loading...
Ummy: Marufuku kutoa rufaa ya matibabu nje
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa agizo kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuhakikisha haitoi rufaa ya matibabu nje ya nchi ikiwa wana uwezo wa kutibu maradhi husika hapa nchini.
Ummy amesisitiza wataalamu kutowaogopa wanasiasa ikiwa wana uwezo wa kumtibu mgonjwa hapa nchini haina ulazima wa kumwandikia rufaa nje ya nchi hata akiwa ni Rais John Magufuli.
Ametoa agizo hilo leo Jumatatu wakati akipokea msaada wa vifaa vipya kwa ajili ya vyumba viwili vya upasuaji vya watoto wadogo na wodi ya watoto ya upasuaji vyenye thamani ya Dola za Marekani 675,000 sawa na Sh1.5 bilioni, kutoka kwa wataalamu na wahisani kutoka nchini Uingereza kupitia taasisi ya Archie Wood Foundation.
"Rais aliponiteua aliniagiza kwamba lazima niachane na rufaa za nje, hatuwezi kuachana nazo ikiwa magonjwa yanayoweza kutibiwa ndani yatatibiwa nje," amesema Ummy.
Amesema Watanzania wana imani na Muhimbili na hivi sasa wengi wanatoka hospitali za kulipia na kufuata matibabu ila changamoto iliyopo ni majengo lakini wapo mbioni kujenga jengo la ghorofa kwa ajili ya wagonjwa wa kulipia.
"Msitoe rufaa ya mgonjwa kama hamjajiridhisha kwamba mnaweza kumtibu hapa hata kama awe Rais, waziri au nani msitoe rufaa kwani maana yake mtakuwa mmeshindwa ni lazima ninyi mseme kwamba hamuwezi na sisi tutashughulikia," amesema.
Amewatahadharisha wataalamu hao na wanasiasa kwamba lazima wahakikishe kweli hawawezi kutibu na kwamba wizara ipo tayari na itawaunga mkono.
Post a Comment