Nairobi, Kenya. Mahakama Kuu ya Kenya imeiamuru Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumjumuisha mgombea urais kwa muungano wa Thirdway Alliance, Ekuru Aukot katika uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26.
Hukumu hiyo imetolewa siku moja baada ya mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa upinzani wa National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga kujiondoa katika uchaguzi huo wa marudio akitoa wito Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuitisha mpya.
Kiongozi huyo wa Nasa amesema uamuzi huo ni kwa maslahi ya Kenya. Waziri Mkuu huyo wa zamani amesema kwa kujiondoa kwake nchi itapata fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu mpya uliohuru na haki kwa mujibu wa sheria.
Uamuzi wa Jaji
Akitoa hukumu leo asubuhi, Jaji John Mativo ameitaka IEBC kurekebisha taarifa ya kwenye Gazeti la Serikali kuhusu idadi ya wagombea urais katika uchaguzi wa marudio na kujumuisha jina la Aukot.
Jaji Mativo amesema Aukot alikuwa sehemu ya waliokuwa wanapinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta kama mtu mwenye maslahi na kesi hiyo.
Jaji amesema haoni sababu kwa nini mrufani asijumuishwe kwenye uchaguzi huo. Pia, amesema kutomjumuisha Aukot kwenye uchaguzi huo utakuwa ukiukwaji wa haki zake.
Tangazo la Gazeti la Serikali liliwataja wagombea wawili Rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake mkuu Raila Odinga. Hatua ya Odinga kutangaza kujiondoa jana na leo mahakama kutoa hukumu inayotaka Aukot ajumuishwe inazidi kutia shaka kuhusu uwezekano wa uchaguzi wa marudio kufanyika kama Mahakama ya Juu ilivyoagiza iliposoma hukumu iliyobatilisha ushindi wa Rais Uhuru katika kesi ya kupinga matokeo ya urais iliyofunguliwa na Odinga.
Loading...
Post a Comment