SIKU chache tu baada ya Rais John Pombe Magufuli kufanikisha kukamilika kwa ufanisi sehemu ya kwanza majadiliano na kampuni ya Barrick Gold kuhusu biashara ya madini hayo nchini, majarida na magazeti mbalimbali maarufu duniani yamemzungia kwa staili tofauti.
Katika makubaliano hayo, huku Mwenyekiti wa Barrick Gold, Prof. John Thornton, akilazimika kusafiri kwa ndege binafsi kuja mara 2 nchini Tanzania, Tanzania imefikia kile ambacho nchi chache sana duniani zimeweza kufanikisha katika kunufaika na sekta ya madini.
Pamoja na kupewa hisa zinazofikia asilimia 16 katika migodi yote ya Barrick nchini, makubaliano hayo pia yanaruhusu Tanzania kuchukua madini yote yanayopatikana baada ya makinikia kuuzwa na itapata faida ya nusu kwa nusu na Barrick baada ya dhahabu ya kawaida kuuzwa.
Aidha, kampuni ya Barrick itaweka ofisi zake mpya katika jiji la Mwanza Tanzania na kwamba idadi ya watanzania wanaoshiriki katika Bodi na menejimenti ya Shirika hilo itaongezeka ili kulinda maslahi ya pande zote mbili.
Ndio maana katika makala yake iliyoitwa “Tanzania’s squeeze on mining firms seems to be working as it gets $300 million in back taxes” Jarida mashuhuri la masuala ya madini Quartz lilimueleza Rais Magufuli kama kiongozi aliyefanikiwa kuyabana makampuni makubwa kwa maslahi ya wananchi wake na hayumbishwi.
“Rais wa Tanzania mwenye msimamo usioyumba katika madini, Dkt. John Pombe Magufuli anaongoza vita inayohakikisha kuwa makampuni makubwa yanapata haki yao lakini wananchi wa Tanzania nao wanapata faida katika sekta ya madini,”anaandika Abdi Latif Dadir mwandishi wa jarida hilo lenye makao yake makuu Marekani.
Kwa upande wake mtandao wa habari za uchumi na biashara wa Bloomberg ulisema kuwa Rais Magufuli ni kiongozi ambaye “anaifanyia mageuzi makubwa sekta ya madini ili kuwafaidisha wananchi.”
Mtandao huo pia umeongeza kuwa licha ya azma hiyo, Serikali ya Magufuli pia ina mikakati mipana zaidi katika “kutekeleza sera ya viwanda na miradi ya kiuchumi katika nchi ya Tanzania ambayo ni ya sita kuwa na uchumi mkubwa katika Ukanda wa Afrika Kusini mwa Sahara.”
Gazeti mashuhuri la New York Times lilianza kwa kusema Serikali nyingi katika nchi za Afrika na Asia-kutoka Afrika Kusini hadi Indonesia zimeanzisha harakati za kuhakikisha zinafaidika zaidi na madai yao.
Gazeti hilo limeeleza hatua mbalimbali alizozichua Rais Magufuli ikiwemo kuzuia usafirishaji wa mchango wa madini maarufu kama makinikia. “Rais wa Tanzania hata hivyo hakusema iwapo uuzaji nje wa madini hayo utaruhusiwa tena ama la,” limeripoti New York Times.
Post a Comment