Wakili Sheck Mfinanga amejitoa kumwakilisha mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema katika kesi ya uchochezi akidaiwa kumkashifu Rais John Magufuli akisema haridhishwi na mwenendo wa shauri hilo.
Mfinanga amejitoa ikiwa ni siku chache baada ya hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia Kisinda aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo kujitoa kutokana na kuwekewa pingamizi na upande wa Jamhuri kuwa ana urafiki na Neema ambaye ni mke wa Lema.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, Desdery Kamugisha, wakili huyo amesema moja ya sababu ni kutokana na upande wa utetezi kutopewa jalada la mwenendo wa kesi licha ya kuwasilisha maombi mara tatu mahakamani hapo.
“Kwa kuwa nimeshaleta notisi ya kukata rufaa naomba iingie kwenye rekodi, najitoa kuendelea kumwakilisha mteja wangu kutokana na kile ninachokiona kisheria kwamba tumeomba proceedings (mwenendo wa kesi) na imeshindikana. Mimi si wakili wake tena, nimejitoa,” amesema.
Baada ya ombi hilo, Mfinanga alikusanya nyaraka zake, alimuaga mteja wake na kunyanyuka kwenye kiti alichokuwa ameketi na kutoka ndani ya chumba cha Mahakama.
Hakimu Kamugisha alimpa nafasi Lema ya kuzungumza naye alisema amemsikiliza wakili wake na hana pingamizi juu ya ombi hilo.
Hata hivyo, amesema kwa ufahamu wake ni kwamba, hii ni mara ya tatu upande wa utetezi umeomba jalada la mwenendo wa kesi lakini hawajapewa na kwa sababu hiyo hana imani na hakimu.
“Mheshimiwa nilishasema sina imani na wewe kama mtu niliyekuwa nimemwajiri kunisaidia katika masuala ya kisheria anaweza kutilia shaka na nilisema hadharani, basi naomba nipewe muda wa kutafuta wakili mwingine,” amesema.
Lema amesema anaomba kupatiwa nyaraka zote za kesi na muda wa kutafuta wakili mwingine.
Baada ya ombi hilo, Wakili wa Serikali, Khalili Nuda alisema ni haki ya kikatiba ya mshtakiwa kuwakilishwa mahakamani. Aliiomba mahakama impatie muda wa kutafuta wakili mwingine.
Nuda ameiomba Mahakama impatie mshtakiwa muda muafaka wa kutafuta wakili mwingine.
Hakimu Kamugisha amesema wakili wa mshtakiwa amejitoa wakati kesi ilipotajwa kwa ajili ya kusikilizwa, hivyo Lema anapewa muda wa kutafuta mwingine. Aliahirisha shauri hilo hadi Novemba 14.
Mwananchi:
Shinda Mamilioni ya Pesa na Meridianbet Leo
18 minutes ago
Post a Comment