Walionusurika ajali ya daladala iliyotumbukia Ziwa Victoria, wamesema iwapo dereva angesikiliza ushauri madhara yasingekuwa makubwa.
Akizungumza katika Hospitali ya Bukumbi Mission wilayani Misungwi alikolazwa, Yohana Ngabula (28) mkazi wa Kijiji cha Buyagu wilayani Sengerema amesema amepoteza mama na dada katika ajali hiyo.
Ngabula amesema walikuwa wakitoka jijini Mwanza kufuatilia mafao ya baba yao katika ofisi za Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
“Nilimshauri dereva agonge hata gari lililokuwa mbele yake badala ya kulielekeza ziwani lakini hakusikia mwisho wake ndiyo hayo yaliyotokea,” amesema.
Amesema baada ya gari kutumbukia ziwani alipasua kioo na kutoka ndipo walipofika vijana wakamuokoa.
Majeruhi mwingine mkazi wa Ibisabageni, Paulo Lazaro ambaye ni mwalimu wilayani Sengerema amesema, “Tulimshauri dereva agonge vitu nchi kavu kuliko kuipeleka gari majini lakini hakusikiliza ushauri wetu, pengine tungepona wengi zaidi.”
Mwalimu huyo amesema alipita dirishani baada ya gari kutumbukia ziwani na kwamba, ana maumivu mabegani na mgongoni.
Mwingine aliyenusurika katika ajali hiyo, Sophia Biambina (32) amesema amepoteza watoto wawili katika ajali hiyo.
Amesema walikuwa wakitoka kwenye msiba wa baba yake wilayani Magu na alikuwa akielekea nyumbani kwake Nyapande wilayani Sengerema.
“Baada ya ajali nilijikuta nimeshatoka nje sikujua nimetokaje, najihisi maumivu makali kwa sababu nilikunywa maji mengi. Kinachoniuma ni kuwapoteza watoto wangu, tulitoka msibani kumzika baba yangu,” amesema.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Bukumbi, Dk Robert Shija amesema walipokea maiti 12 na majeruhi hao watatu.
Amesema walipokea miili ya Joseph Paulo, Rehema Makalanga, Mariamu Kagosha, Pendo Msafiri, Salome Msafiri, Joyce Hamadi, Martha Makenzi, Gwanchele Mswagi na Kazungu Lukuba wote wakazi wa Wilaya ya Sengerema.
Wengine ni Martine Kamlamo mkazi wa Bukumbi, Hamadi Zahalaki wa Bukoba na Ally Abdul wa Kayenze wilayani Ilemela.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda ameuagiza uongozi wa hospitali kuwa, ndugu watakaoshindwa kusafirisha miili wawasiliane na ofisi ya wilaya kwa ajili ya kupata msaada.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole amesema walipanga kuisafirisha miili hiyo lakini tayari ndugu wameshaichukua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema hakuna miili mingine ambayo imeopolewa lakini Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kimerudi eneo la tukio.
Msangi alisema jana Jumatatu kuwa hawajapata idadi kamili ya watu waliokuwemo kwenye gari hilo.
Post a Comment