Profesa wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benson Bana
Dar es Salaam. Wakati wimbi la viongozi wa kuchaguliwa kuhama vyama vyao na kulazimu kufanyika kwa uchaguzi mdogo likiendelea, Profesa wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benson Bana amesema hali hiyo inaonyesha ni kwa namna gani ambavyo hawajui ni kwa nini walijiunga na vyama hivyo na nini wanapaswa kukisimamia.
Alisema hayo alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu hamahama ya viongozi wa kisiasa, “Hawajui nini kiliwapeleka kwenye hivyo vyama, niseme tu hii hali si nzuri na inatokana na wengi kuingia kiushabiki tu na si imani kwa chama walichoamua kugombea.”
Profesa Bana alisema hamahama hiyo inaweza kumalizwa na sera ya mgombea binafsi endapo hilo litafanyika nchini.
Hivi karibuni, aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu alitangaza kuachana na CCM na kujiunga na Chadema hivyo kupoteza ubunge.
Pia, juzi diwani wa Kihesa, Manispaa ya Iringa, Edgar Mgimwa aliihama Chadema na kujiunga na CCM wakati wa mkutano wa kampeni wa chama hicho katika Kata ya Kitwiru ambayo pamoja na Kimala iliyoko Kilolo, zitafanya uchaguzi wa marudio Novemba 26.
Diwani huyo anaungana na wenzake watatu waliohama Chadema miezi kadhaa iliyopita akiwamo Baraka Kimata anayewania tena udiwani katika Kata ya Kitwiru, safari hii kupitia CCM.
Wengine ni waliokuwa madiwani wa viti maalumu, Leah Mleleu na Husna Daudi ambao baada ya kujiuzulu walisema wangebaki kuwa wanachama wa Chadema lakini katika mkutano huo wa CCM juzi, nao walitangaza kujiunga na chama hicho na kupokewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole.
Jana, Mgimwa alisema moja ya sababu za kuhama Chadema ni kile alichokiita udikteta wa Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Alisema kutokuwapo maelewano baina ya mbunge huyo na mmoja wa viongozi wa Wilaya ya Iringa, kunasababisha kuzorota kwa maendeleo jambo ambalo alisema haliungi mkono.
Hata hivyo, Msigwa alisema jana kuwa, Chadema haibabaishwi wala kuyumbishwa na hatua ya Mgimwa kuhama huku akidai kuwa huo ni mwendelezo wa baadhi ya madiwani kununuliwa.
“Ukiwa vitani, inapotokea askari anaanguka huna haja ya kugeuka nyuma kwa sababu hafanyi jeshi zima kuyumba, sisi tunasonga mbele; na kwa sababu tunajua ni mpango wa kutengeneza, hatuna wasiwasi katika hilo,”
Alisema Chadema inachokifanya sasa ni kujipanga kwenye uchaguzi mdogo ili kurejesha kata ilizokuwa inazishikilia.
Alisema kwa sababu kata zinazoachwa wazi zitaitishwa uchaguzi mdogo, kazi yao itakuwa kuhakikisha wanashinda kwa kishindo.
CCM Iringa wazungumza
Katibu wa Itikadi, Hamasa na Uenezi wa CCM Manispaa ya Iringa, Edol Bashiri alisema wataendelea kuwapokea madiwani wengine wanaohamia chama hicho kwa kuwa milango ipo wazi.
“Wanafuata sera safi na demokrasia inayoendeshwa kwa vitendo, tunaendelea kuwakaribisha wengine wanaotaka kuja na tutaendelea kuwapokea,” alisema.
Bashiri alisema wanaendelea kufanya kampeni na kwamba, wapo wanachama wengine wanaohamia CCM wakitokea Chadema.
on Tuesday, November 7, 2017
Post a Comment