Oktoba 30, 2017 Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu atangaza kujivua Ubunge wa Jimbo hilo. Amesema CCM imepoteza uelekeo na kuomba Wanachama wa CHADEMA kama wataona inafaa wamkaribishe.
Nyalandu ametoa sababu zilizomfanya ahame na Watu wengineo nao pia wametoa sababu za kuhama kwa Nyalandu lakini ukweli unabaki palepale Nyalandu ametumia haki yake ya msingi kabisa ya kwenda sehemu anayoamini ni sahihi kwake.
Hama hii ya Nyalandu haiwezi kuleta madhara yeyote kwa Chama Cha Mapinduzi ama kwa Serikali kwa sababu si mara ya kwanza kwa Wanachama au waliokuwa viongozi waandamizi wa chama na Serikali kuhama CCM lakini bado CCM ikaendelea kuwa imara.
CCM imeshapita kwenye majaribu mazito kadhaa lakini bado ikaendelea kuwa imara kabisa. Tuweke sawa kumbukumbu. Mathalani mwaka 1968, aliyekuwa Katibu Mkuu wa TANU na wa pekee, Oscar Kambona ; aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza wa UWT, Bibi Titi Mohammed; Katibu Mwenezi wa TANU, na Mbunge wa Geita Mashariki, Fortunatus L.Masha; Katibu Mkuu wa TANU Youth League “TYL” na Mbunge wa Rungwe , Elli Anangisye walifukuzwa ndani ya chama kutokana na utovu wa nidhamu ukiwamo na kutuhumiwa kwa kutoliafiki azimio la Arusha waliloshiriki kulipitisha. Kwa tuhuma hiyo, Halmashauri Kuu (T) ya TANU ilipokaa Tanga haikutaka ushahidi zaidi wa juu ya uwaminifu wao katika chama, zaidi ya kuwafukuza ndani ya chama lakini TANU.
Tuendelee kukumbuka sakata la Seif kufukuzwa na wenzake sita mwaka 1987 lakini CCM ikaendelea kuwa imara na kushika hatamu zaidi.
Halikadhalika aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba kuvuliwa wadhifa mwaka 1994 kutokana na kauli yake aliyoisema ya kuwa CCM imepoteza dira. Katibu Mkuu CCM alitimuliwa lakini bado Chama kiliendelea kuwa imara kabisa na kushinda kwa kishindo uchaguzi mkuu wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995 na hatimaye kushika dola.
Tusisahau sakata la Rais wa pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe la kutaka Muungano uvunjwe na katiba ya nchi ibadilishwe, hali iliyochafua hali ya hewa visiwani Zanzibar. Kitendo hicho kilimkera sana Mwasisi wa Muungano na baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na kuamua kumpa adhabu kali Mzee Jumbe, hali iliyozua kizaazaa lakini mwishowe CCM iliendelea kuwa imara na kushinda uchaguzi na kuendelea kushika dola.
Pia tuendelee kukumbuka sakata la kundi la G55 na hatma ya uongozi wetu. G55 lilikuwa ni kundi lililoibuka Bungeni miaka ya 1990 hadi 1992 lililokuwa na nguvu kubwa sana lililokuwa likidai Serikali 3. Kundi hili lilikuwa likiongozwa na viongozi wazito ndani na nje ya Bunge kama akina Njelu Kasaka, Philipo Marmo, Masumbuko Lamwai na wengineo lilizua mtikisiko mkubwa lakini hekima na busara za Mwalimu Nyerere zilisaidia kutuliza hali ya hewa. Licha ya mazito hayo lakini bado CCM iliendelea kuwa imara, kushinda chaguzi na kushika dola.
Tuendelee kukumbuka dhoruba kali lililotokea mwaka 2015 kwenye uchaguzi mkuu uliopelekea Mawaziri wakuu wastaafu wawili na viongozi wazito waandamizi wa Serikali na chama kuhama CCM na kujiunga na chama cha upinzani lakini mwisho wa siku CCM iliendelea kuwa imara, ikashinda vita ya uchaguzi na hatimaye kushika dola.
Suala la kuhama kwa Nyalandu lisiwe gumzo la kupelekea baadhi ya watu kumuweka kwenye level tofauti ya juu sana kisiasa na kuishusha hadhi CCM na Serikali yake. Wakati wakiyafikiria hayo wajiulize wako wapi waliohama kwa mbwembwe mwaka 2015? Wako wapi waliotikisa sakata la G55? Kati yao na CCM nani anaendelea kuwa lulu? Ukipata majibu ya maswali hayo utagundua kuhama kwa Nyalandu si lolote, si chochote!!
Nyalandu si wa kwanza, wala si wa mwisho kuihama CCM. Nyalandu ametumia haki yake ya kikatiba kabisa ya kuchagua anachotaka lakini anapokosea yeye ni kuondoka na kuanza kushusha kebehi na lugha za kuudhi kwa kusema CCM na Serikali ya sasa imepoteza dira. Kwa kauli hii, unadhani wana CCM watakaa kimya wasimshambulie Nyalandu? Angeondoka kimya kimya bila lugha ya kuudhi angepungukiwa na nini?
Nyalandu anaposema CCM imepoteza dira nashindwa kuielewa hiyo dira yake anayoimaanisha. CCM anayodai imepoteza dira ndio hiyo hiyo inayoisimamia Serikali inayotoa elimu bure kuanzia shule ya msingi, hadi Sekondari; ndio Serikali inayotoa mikopo ya elimu ya juu kwa Wanafunzi wanaostahili; inayofuta kodi na kuboresha kilimo nchini; Inayonunua vifaa tiba na madawa hospitalini; Inayojenga hostel za wanafunzi; Inayonunua ndege 6 mpya; Inayojenga reli ya kisasa ya standard gauge; Inayosimamia rasilimali madini ziwanufaishe watanzania wote; Inayojenga miundombinu na kuboresha huduma za kijamii kila sehemu nchini; Inayoboresha mapato ya ndani na mengineyo kibao.
Kwa hayo baadhi tu ya machache niliyoyataja yanayoonyesha Matokeo chanyA+ ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi. Hivi utasemaje CCM hii imepoteza dira? Utasemaje Serikali hii imepoteza dira? Haoni uelekeo wa CCM?
Kwa hayo baadhi tu ya machache niliyoyataja yanayoonyesha Matokeo chanyA+ ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi. Hivi utasemaje CCM hii imepoteza dira? Utasemaje Serikali hii imepoteza dira? Haoni uelekeo wa CCM?
Nyalandu ni lazima ajiulize yuko wapi Lawlence Masha, yuko wapi Kingunge, yuko wapi Mgeja, yuko wapi James Lembelii, yuko wapi Sumaye? Inabidi awatazame hawa walipo, naye atajua atakapokuwepo katika hali na nafasi ya kisiasa nchini.
Emmanuel J. Shilatu
01/11/2017
01/11/2017
Post a Comment