Na Bashir Yakub.
Kuna mambo ambayo yafaa tujihadhari nayo sana hasa kipindi hiki. Wengi wamefutiwa umiliki wa ardhi. Takwimu za kufutiwa ni kubwa sana kipindi hiki kama ulikuwa hujui. Kwa watu wanaonunua ardhi na kwenda kuishi nje ya nchi hili lawahusu sana kabla hamjapoteza ardhi zenu.
Najua unachojua kuhusu kutelekeza ardhi ni pengine kutokujenga, au kutoitumia kama ilivyopangiwa matumizi, nk. Ni kweli lakini hiyo ni maana finyu ya kutelekeza ardhi. Maana ni zaidi ya hiyo, na hapa tutaona ili ujihadhari na uwezekano wa kupoteza ardhi yako.
1.MAMBO AMBAYO UKIFANYA UTAHESABIKA KUTELEKEZA ARDHI.
Mambo haya yameelezwa na Sheria Namba 4 ya ardhi ya 1999 kifungu cha 51(1).
( a ) Kutokulipa kodi, tozo au ushuru wowote ambao upo kisheria kwa ajili ya ardhi ni kutelekeza ardhi kwa mujibu wa sheria hiyo. Mnazijua kodi za majengo, kodi za ardhi nk. Hizi ni muhimu sana na kimsingi ndizo zinazoeleza uhai wa ardhi yako.
Ikiwa hulipi hizi hata kama eneo hilo umejenga kiwanda kinachofanya kazi saa 24 siku 7 za wiki bado mbele ya macho ya sheria unahesabika kutelekeza ardhi. Dawa ya kuepuka hili ni ndogo. Lipa hizo kodi na tozo kwa mujibu wa sheria. Yamkini hizi huwa si pesa nyingi sana ya kumshinda mmiliki kulipa.
( b ) Jengo ndani ya ardhi kuwa gofu ni kutelekeza ardhi kwa mujibu wa sheria. Lakini pia katika eneo hilo sheria imetumia neno “disrepair”. Maana yake kutokufanya ukarabati. Kwa tafsiri hii ni kuwa kumbe hata kutokufanyia majengo yetu ukarabati nako ni kutelekeza ardhi.
Utaona katikati ya miji yetu majengo ya zamani machafu, yaliyopauka. Japo ndani mwake watu wanaishi na maofisi yamo bado kwa tafsiri ya neno “disrepair” ni kuwa jengo hilo limetelekezwa. Na sheria imeeleza zaidi kuwa itakuwa mbaya zaidi ikiwa jengo hilo linahatarisha afya au maisha ya watumiaji wake , majirani au hata wapita njia.
KUSOMA ZAIDI sheriayakub.blogspot.com
Post a Comment