WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea wanachama wapya 37 kutoka vyama vya CUF na CHADEMA ambao wameamua kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kwa mujibu wa Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Bw. Barnabas Essau wanachama 35 kati ya hao wametoka CUF na wawili wametoka CHADEMA.
Wanachama hao walipokelewa jana (Jumapili, Novemba 5, 2017) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mbekenyera, wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
Bw. Essau alisema wanachama hao wote wametoka kata za Mbekenyela na Matambalale. Walikabidhiwa kadi mpya za CCM, na kula kiapo cha uaminifu.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wenzake wapya, Bw. Mohammed Issa Ndogoro ambaye amehamia kutoka CHADEMA, alisema wamejiunga na CCM baada ya kuridhishwa na mwelekeo wake. Alisema wameguswa na jinsi Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dk. John Pombe Magufuli inavyofanya kazi ya kutatua kero za wananchi.
Alisema amekaa upinzani kwa miaka 23 lakini anaikubali CCM sababu ya uwazi wake na ameshangaa kuona akipewa kadi na stakabadhi ya walipo yenye jina lake, jambo ambalo hajawahi kuliona katika vyama vingine vya upinzani.
“Sote sisi tumehamia CCM, uhai wa chama ni michango. Nani aseme hapa kama aliwahi kupewa stakabadhi katika chama chake, na kama yupo nampa sh. 5,000/- sasa hivi,” alisema Bw. Ndogoro na kuamsha kicheko kwenye mkutano huo.
Post a Comment