Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

YA DK. MAGUFULI, APEWE DK. MAGUFULI



YA DK. MAGUFULI, APEWE DK. MAGUFULI

Mungu Mtukufu pale anapokusudia kuyapitisha mambo yake, kudra zake, neema na baraka zake hata kama Walimwengu watakaa na kupanga njama au mikakati ya kuyazuiya ile yasiwe yatawashinda na kujikuta  yaliokusudiwa yakijiri.

Watanzania tuliobatika kuziona tawala toka awamu ya kwanza, pili, tatu, nne na hii ya tano, tunazijua vyema tawala zote zilivyoendeshwa. Changamoto zake, tija, vikwazo na mafanikio aidha ya kisiasa. kiuchumi na kijamii.

Tumeona jinsi Serikali ya Mwalimu Julius Nyerere ilivyojenga misingi ya utaifa, miiko ya uongozi , uzalendo na kuwaunganisha wananchI hatimaye kuwa na umoja wa kitaifa na mshikamano.

Utawala wa Mwalimu Nyerere umejenga viwanda, ukaanziaha mashirika ya umma, wakala za Serikali, mashamba ya Serikali na kampuni za Serikali,kuanzisha Benki ya Taifa (NBC) na Benki iliowalenga wakulima wajiinue kiuchumi na kimaendeleo  (CRDB) .

Hata hivyo Watu /Viongozi waliopewa dhamana za kuongoza /kusimamia masuala hayo walikosa mioyo ya uzalendo kwani hawakutaka kuwa wakweli na waaminifu, badala yake wakashiriki hujuma za kiuchumi, wizi na ubadhirifu.

Wakati utawala wa awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi ulipoingia madarakani ulikuta mambo yakiwa shaghalabaghala, mzobe mzobe, ndembendembe  huku mzigo wa uendeshaji ukiitegemea ruzuku toka Serikali kuu.

Viwanda, mashirika, kampuni na wakala za Serikali zikayumba na mambo yakaelekea kuvurugika zaidi ikichangiwa na kushiriki kwetu katika harakati muhimu za ukombozi kusini wa Afrika na vita vya Kagera wakati wa awamu ya kwanza.

Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa katika utawala wake ukakumbwa na vikwazo vya kisera kimataifa pia ikakutana na mwanzo wa sera za ubinafsishaji, kuenea na kutawandawaa kwa utandawazi ikiwemo na  kushamiri kwa nguvu za soko huria.

Viwanda, mashirika ya umma. baadhi ya kampuni na taasisi kadhaa, zilalazimika kubinafsishwa na baadhi kuendeshwa kwa ubia uliokuwa hafifu  huku Serikali ikipata faida haba ambazo hazikukidhii mahitaji  na haja za kiuchumi.

Rais Mkapa kajitahidi kwake kubuni  na kuibua mambo mapya, akaanzisha miradi ya maendeleo ya elimu ya msingi na sekondari yaani  MMEM na MMES pia mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF) ambao licha ya kuzisaidia kaya masikini, ukaendeleza miradi ya elimu, maji, kilimo, Zahanati, ufugaji na barabara za vijijini .

Kuingia kwa Rais wa awamu ya nne akakutana na changamoto nyingi ikiwemo za ongezeko la watu, uhaba wa Shule za Msingi na Sekondari, maabara, nyumba za kuishi Walimu , Waganga na Wauguzi na ukosefu wa vitendea kazi kwa wataalam wa ugani .

Hata hivyo takwimu zinaonyesha kuwa ndiyo Serikali ilipeleka fedha nyingi za ruzuku kwenye Serikali za mitaa kuliko wakati mwingine uliopita kwa lengo la kuimarisha huduma za jamii.

Fedha hizo karibu robo tatu yake zilitafunwa na mchwa kwenye Halmashuri za wilaya,kudumaza kwa maendeleo na wachache wakijitajirisha huku maskini wakiteseka vijijini kwa kukosa huduma muhimu.

Si hivyo  tu itakumbukwa kuwa ndiyo utawala ulioondoshwa tatizo la ukosefu wa madaraja na ulioungaisha mtandao wa barabara wa nchi nzima na kujengwa kwa kiwango cha lami lakini pia ukajenga uchumi imara na kupunguza mfumuko wa bei .

Katika utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Dk John Magufuli kwa mukhtasari ndiyo uliobeba changamoto zote, uchafu, vikwazo na mafanikio yaliyogubikwa toka awamu ya kwanza hadi ya tano.

Amekutana mikataba mobovu, ukusanyaji mzuri wa mapato yaliokuwa yakipoteza fedha nyingi na kuingia mifukoni mwa watu wachache kwa lengo la kuihujumu serikali.

Pamoja na yote kufanyika katika awamu ya kwanza hadi ya nne, wajibu wa wananchi wote sasa ni kutomkatisha tamaa Rais badala yake tuungane naye,tusimame naye pamoja pia tumsaidie

Ni wajibu wetu kumtakia  kwa Mwenyezi Mumgu  awe kiongozi imara asiwe mwenye kulalama, moyo wake tusiupige fundo, tumIudishie stahamala  na kumfanya awe mtu wa matendo na vitendo.

Mungu amzidishe ari ya kujenga jukwaa jipya la uzalendo na utaifa, subira na uvumilivu ili anayoyataka yaweze kufikiwa kwani siku zote subira huvuta kheri. Anayoyafanya Rais Dk Magufuli  hayana faida binafsi kwake ila ni kulitakia mema Taifa

Anayoyakusudia na kutaka kuyasimaia sasa naamini iko siku yatajiri na kudhihirika kwa vitendo na ushahidi pia kuwanufaisha wananchi wote huku wale wanaombeza sasa ndiyo watakaokuwa wa kwanza kumshamgilia.

Ameanza vyema ikiwa ni pamoja na kujenga nidhamu na uwajibikaji kwa Watumishi wa umma hali iliyopelekea vitendo vya rushwa na ufisadi kupungua nchini. Matumizi ya anasa maofisini, safari za nje nazo pia zimepungua hali inayosababishwa pesa nyingi kuokelewa na nyingi kupelekwa kwenye matumizi ya kimaendeleo.

Rais Magufuli ameanza kwa kasi ya kuhakikisha kila penye upenyo ama mianya ya upotevu wa fedha panazibwa. Amefanya hivyo Bandarini kwenye Makontena, mafuta, ushuru akaenda kwenye Mamlaka ya mapato Tanzania na hatimaye kuzaa matunda ya mapato kuongezeka kutoka Tsh. Bilioni 800 hadi Trilioni 1.5 kwa mwezi.

Mapato ya ndani kuimarika yakapelekea Serikali kuanza mara moja kutoa Elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari kwa kugharamikia zaidi ya Tsh. Bilioni 23 kwa mwezi; Serikali ya Rais Magufuli imeendelea kukidhi haja ya kuhakikisha kila shule kuna madawati ya kutosha, kuna makataba na maabara za kutosha. Mambo haya yalikuwa changamoto kubwa awamu zilizopita lakini ndani ya miaka 2 ya utawala wa JPM yamebaki historia.

Serikali ya Rais Magufuli kwa kutumia pesa za ndani pekee imefanikiwa kununua ndege 6 mpya za abiria. Rais Magufuli ameendelea kufufua Mashirika ya umma kwa kuhakikisha ujenzi wa reli kwa kiwango cha standard gauge ambayo itakuwa reli ya kisasa kabisa ya abiria na mizigo yenye spidi kali itakayoanzia dare s Salaam malengo ifike Kigoma na Mwanza lakini hatua ya ujenzi wa awali ni ifike Morogoro.

Rais Magufuli ameendelea na kazi ya kuhakikisha miundombinu ya kisasa inajengwa. Mathalani, viwanja vya ndege, madaraja, vivuko na barabara zikiwemo flyovers mbili za kisasa za Tazara na Ubungo.

Rais Magufuli ameendelea kuhakikisha azma yake ya kuwa Tanzania ya Viwanda inatimia na matunda yake tunaona yanatimia. Karibu kila mkoa nchini Tanzania unashindana kuhakikisha sera ya Taifa ya Viwanda inatimia. Viwanda hivi vitakuwa chachu ya kupunguza tatizo la ajira nchini, kuimarisha mapato binafsi na ya Taifa na hata uimarishwaji wa huduma za kijamii maeneo ya viwanda kuimarika. Sera ya viwanda imefanikiwa nchini kutokana na Serikali kupunguza ama kufuta vikwazo vya urasimu kwa Wawekezaji hapa nchini.

Rais Magufuli ameendeleza jitihada za kuhakikisha Tanzania inakuwaje na umeme wa u hakika kwa kujenga vituo viwili vya umeme vya Kinyerezi I na II ili kuendana na kasi ya Tanzania ya viwanda.

Uzalendo uliotukuka alionao Rais Magufuli umesababisha Tanzania kutokugeuzwa tena kuwa shamba la Bibi kwa kuhakikisha rasilimali madini zinawanufaisha Watanzania ambapo kuanzia sasa Tanzania itakuwa na hisa 16%, tutagawana faida kwa 50/50, Kiwanda cha kuchenjua kitajengwa hapa nchini na hivyo kuepusha michanga ya madini kusafirishwa nje ya nchi, akaunti za wachimbaji wakuu kuwa hapa nchini na mengineyo mengi. Haijawahi kutokea! Hakika Uzalendo wa Rais Magufuli umeliokoa Taifa kupata manufaa ya rasilimali madini.

Utawala wa Rais Magufuli umeleta neema kwa Wakulima na kilimo nchini kwa kufanikiwa kufuta kodi mbalimbali kandamizi kwenye sekta ya kilimo, kusimamia hakuna biashara ya rumbesa, kusimamia stakabadhi ghalani, kusimamia masoko ya mazao, kusimamia Wakulima wapate malipo yao kwa wakati toka kwa Wafanyabiashara ama wanunuzi. Mathalani, Leo hii Wakulima wa Korosho hawaamini macho na masikio yao wanapoona bei ya korosho imepanda kutoka Tsh. 800 kwa kilo moja mpaka Tsh. 3850 kwa kilo moja. Tangu Dunia iumbwe Wakulima wa Korosho Tanzania hawajawahi kuuza kwa bei kubwa mno namna hiyo, imewezekana kwenye utawala wa Rais Dk. John Pombe Magufuli.

Rais Magufuli ameendelea kupambana vikali dhidi ya adui “Maradhi” kwa kuhakikisha Madaktari na Wahudumu wa Afya wanakuwepo wa kutosha; Kuhakikisha Watoto chini ya miaka 5, Wazee zaidi ya miaka 60 wasiojiweza waanapatiwa bima za afya za matibabu bure kabisa; Huduma ya Mjamzito na kujifungua imeboreshwa kwa kiwango cha hali ya juu; Kuhakikisha Madawa na vifaa tiba Hospitalini vinapatikana kwa wingi. Mathalani Serikali ya Rais Magufuli iliagiza vitanda vya kutosha, iliagiza mashine za vipimo na pia imehakikisha inajenga maduka ya madawa ya MSD  ndani ya kila hospitali ambapo sasa madawa yanapatikana kwa bei nafuu kabisa.

Hakika ni miaka miwili ya ufanisi wa kiutendaji wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi uliotukuka, miaka miwili ambayo Watanzania tumeanza kuona Matokeo chanyA+. Rais Magufuli ameonyesha nia ya dhati, uchapakazi, Uzalendo, hekima na busara katika uongozi wa utawala wake. Jukumu letu Watanzania ni kushikamana nae, kumuunga mkono, kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuheshimu sheria, Taratibu na Kanuni za nchi. Tukiyazingatia haya, Tanzania Mpya yenye maendeleo tunayoyataka inawezekana.

Na Emmanuel J. Shilatu
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top