Mkuu wa Mkoa wa Manyara mstaafu, Joel Bendera amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Msemaji wa MNH, Aminiel Aligaesha amesema, “Ni kweli Joel Bendera amefariki. Aliletwa leo na gari la wagonjwa saa 6:30 mchana na ilipofika saa 10:24 jioni alifariki.”
Aligaesha amesema Bendera alipokewa hospitalini hapo akitokea Bagamoyo mkoani Pwani.
Kuhusu chanzo cha kifo chake Aligaesha amesema, ‘’Hilo sasa ni suala la familia lakini kwa wakati huu itoshe kusema amefariki.”
Bendera pia amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Mbali ya ukuu wa mkoa, amewahi kuwa mbunge wa Korogwe Mjini na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo katika utawala uliopita wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.
Katika mabadiliko ya wakuu wa mikoa yaliyofanywa na Rais John Magufuli Oktoba 26,2017, Bendera alikuwa miongoni mwa waliostaafu.
Nafasi yake imechukuliwa na Alexander Mnyeti aliyepandishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara akitokea kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru.
Post a Comment