Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amesema yuko tayari kuendelea kukitumikia chama hicho.
“Neno la mwenyekiti kwangu ni amri kama umeona bado unahitaji niendelee kukusaidia niko tayari kufanya hivyo,” amesema Kinana leo Jumatatu Desemba 18,2017 katika mkutano mkuu wa CCM unaoendelea mjini Dodoma.
Kinana ametoa kauli hiyo wakati kukiwa na minong’ono kuwa ameandika barua akiomba kuachia nafasi yake ya ukatibu mkuu.
Awali, Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli aliweka wazi kuwa Kinana amekuwa msaada mkubwa katika kukiongoza chama hicho.
“Mzee Kinana amenisaidia sana. Amenisaidia mno kwenye kufanya mabadiliko ndani ya chama na ni mategemeo yangu ataendelea kunisaidia,” amesema.
Katika hatua nyingine, Kinana ametoa siri ya ushindi wa kishindo wa chama hicho katika uchaguzi kuwa ni kutokana na ilani bora, demokrasia na kusikilia maoni ya wanachama.
Kinana amesema demokrasia imekuwa msingi wa chama hicho ndiyo sababu kinaimarika.
“CCM tunazingatia demokrasia, wanachama wapo huru kutoa maoni ndani ya chama. Hili linafanyika kwa kuwa usipowapa uhuru wa kusema ndani watasema nje,” amesema.
Post a Comment