TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Mimi Mackdeo Mackeja Shilinde mdau na Mwanachama wa chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), leo tarehe 05 Desemba 2017, nimepeleka barua kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) nikiiomba ofisi yake kufanya Ukaguzi maalum kwa chama chetu (SPECIAL AUDIT)kuhusiana na pesa za ruzuku na matumizi yake ili kuondoa utata unaokikumba chama chetu kwa kipindi kirefu sasa kuhusiana na masuala ya kifedha.
Nyote mnafahamu kwamba chama chetu ni miongoni mwa vyama vya siasa vinavyopokea pesa za ruzuku kutoka serikalini kila mwezi ambapo kwa chama chetu tunapokea zaidi ya
milioni 300 kwa mwezi.
Kadharika, nyote ni mashahidi kuwa pesa za ruzuku ni pesa zinazotokana na kodi za
wananchi wengi wao wakiwa walalahoi na hivyo ni vyema matumizi na usimamizi wake uwe wazi bila vificho.
Kuibuka kwa manung’uniko miongoni mwetu wanachama kuhusiana na matumizi ya
Ruzuku ya chama chetu, ikiwemo viongozi wetu wa kitaifa na kanda mbalimbali za chama,
kulipana mishahara minono, posho zisizozingatia mgawanyo rasmi na kuzagaa kwa taarifa ya kwamba mwenyekiti wa chama amekuwa akikidai chama zaidi ya shilingi bilioni saba (7,000,000,000/=) pesa anazodai kuwa alikikopesha chama kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na hivyo kwa zaidi ya miaka miwili sasa amekuwa akijilipa deni hilo jambo ambalo si sahihi na kinyume cha taratibu, kushindwa kupelekwa ruzuku mikoani na wilayani kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za chama ndiko kunakotusukuma kuomba uchunguzi maalum.
Mimi na wanachama wenzangu kutoka mikoa zaidi ya kumi na mbili, tumekubaliana
kutafuta ukweli wa matumizi hayo ya pesa hizo za ruzuku kwa kutumia njia halali za kisheria ambapo mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali ndio taasisi yenye mamlaka ya kufanya ukaguzi wa kimahesabu hasa katika pesa zinazotokana na umma.
Nakala ya barua hiyo tumeipelekaTAKUKURU na Ofisi za Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini.
Imetolewa na Mackdeo Makeja Shilinde
Mwanachama Mwandamizi – CHADEMA,
+255685072359
Shilinde.mackeja@gmail.com
Post a Comment