Jeshi la Polisi nchini limetamba kushinda vita dhidi ya uhalifu baada ya kupunguza matukio ya aina hiyo huku likikiri kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji na kunajisi.
Wakati hali ikiwa hivyo, jeshi hilo limetoa tahadhari kwa watu ambao hujihusisha na uhalifu hasa katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka kwa lengo la kutaka kujipatia kipato kwa njia zisizo halali kuwa watachukuliwa hatua kali kwa kuwa limejipanga kupambana nao.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hali ya usalama nchini.
Alisema hali ya usalama wa nchi kwa ujumla ni ya kuridhisha na kwamba takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia Januari hadi Novemba, mwaka jana, makosa makubwa ya jinai yalikuwa 68,204 ikilinganishwa na makosa 61,794 yaliyoripotiwa mwaka huu.
Hali hiyo imesababisha upungufu wa makosa 6,410 ambayo ni sawa na asilimia 9.4.
Ubakaji Waongezeka
Hata hivyo, Kamishna Boaz alisema makosa ya ubakaji na kunajisi yanaonekana kuongezeka kwa kuwa kwa mwaka 2016 hadi kufikia Novemba, yaliyoripotiwa yalikuwa 6,935 kulinganisha na makosa 7,460 ambayo yaliripotiwa mwaka huu.
“Hili ni ongezeko la makosa 478 sawa na asilimia 6.8 wakati makosa ya kunajisi yalikuwa 16 mwaka 2016 ikilinganishwa na makosa 25 ambayo yametokea mwaka huu na kufanya ongezeko la makosa tisa sawa na asililimia 56.3,” alisema.
Alisema kuna sababu tatu ambazo zimechangia kuongezeka kwa matukio hayo ikiwamo mmomonyoko wa maadili kwa kuwa kuna watu wanaparamia watoto wadogo. Pia alisema hali hiyo inachangiwa na ushirikina kutokana na baadhi ya watu kuambiwa kuwa wakitembea na watoto wadogo wanaweza kufanikiwa katika mambo fulani, lakini wakati mwingine hiyo inatokana na tamaa za mwili.
“Sasa sababu hizo ni kwamba tiba yake ipo kwenye jamii na sisi tutaweka msisitizo sana mwakani na pengine mwisho wa mwaka kuhusiana na matukio hayo,” alisema Boaz.
Makosa dhidi ya Binadamu
Alisema makosa dhidi ya binadamu ambayo yanajumuisha mauaji, kubaka, kulawiti wizi wa watoto, kutupa watoto, kunajisi na kusafirisha binadamu yaliyoripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Novemba, 2016 yalikuwa 11,513 kulinganisha na 11,620 yaliyoripotiwa mwaka jana ambayo ni ongezeko la makosa 107 sawa na asilimia 0.9.
Pia alisema makosa ya wizi wa silaha, unyang’anyi katika barabara kuu, unyang’anyi wa kutumia silaha, unyang’anyi wa kutumia nguvu, uvunjaji, wizi, wizi wa pikipiki, wizi wa magari, mifugo pamoja na kuchoma nyumba moto mwaka jana yaliripotiwa 34,830 wakati mwaka huu yameripotiwa makosa 29,677 ambayo ni pungufu kwa makosa 5,153 sawa na asilimia 14.8.
Makosa ya uhalifu wa kifedha
Boaz alisema makosa ya noti bandia , wizi katika mabenki, wizi katika mashirika ya umma, wizi katika vyama vya ushirika na makosa ya kughushi jumla ya yaliripotiwa makosa 1,861 kwa mwaka jana ukilinganisha na mwaka huu yaliripotiwa makosa 1,526 ikiwa ni pungufu ya makosa 335 sawa na asilimia 18.0.
Kwa upande wa uhalifu katika jamii, alisema makosa hayo ni yale ambayo yanahusisha kupatikana na silaha, dawa za kulevya, bangi, mashamba ya bangi, mirungi, nyaraka za serikali, magendo, rushwa, uvuvi haramu, kupatikana na mazao ya bahari na wahamiaji haramu.
Alisema makosa ya aina hiyo yaliyoripotiwa kwa kipindi cha Januari hadi Novemba, mwaka huu yalikuwa 20,000 kulinganisha na makosa 18,971 yaliyoripotiwa mwaka jana.
Makosa ya Barabarani
Kuhusu makosa ya usalama barabarani, alisema mwaka jana kuanzia Januari hadi Desemba yaliripotiwa matukio 9,550 ikilinganishwa na 5,537 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka huu ikiwa pungufu ya matukio 4,013 sawa na asilimia 42.
Boaz alisema ajali hizo zilisababisha vifo vya watu 3,108 na majeruhi 8,898 kwa mwaka 2016 wakati mwaka huu watu waliokufa ni 2,491 na majeruhi 5,696.
“Uchunguzi umebaini kuwa kiasi kikubwa, ajali zinasababishwa na vyanzo vikuu vitatu ambavyo ni sababu za kibinadamu, ubovu wa vyombo vya usafiri na sababu za kimazingira.
“Sababu za kibinadamu ni pamoja na uendeshaji wa hatari, uzembe wa madereva, uzembe wa abiria, mwendokasi, uzembe wa watembea kwa miguu, ulevi, mifugo isiyochungwa na uzembe wa waendesha pikipiki,” alisema.
Aidha, alisema katika msimu wa sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, wamejipanga vyema kudhibiti vitendo vyote vya uhalifu vitakavyojitokeza kwa kuwa ulinzi utaimarishwa katika maeneo yote ikiwamo kwenye nyumba za ibada, fukwe za bahari, sehemu za starehe na mengine ya mikusanyiko mikubwa ya watu.
Post a Comment