Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na viongozi wa kampuni ya Total ambayo ni mwekezaji mkubwa wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania na kuwahakikishia kuwa Tanzania itatoa ushirikiano wa kutosha kwa kampuni hiyo na washirika wengine katika ujenzi wa mradi huo.
Viongozi wa Total waliokutana na Mhe. Rais Magufuli jana tarehe 05 Desemba, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam ni Rais wa masoko na huduma Bw. Momar Nguer, Rais wa Total Afrika Bw. Stanislas Mittelman, Makamu wa Rais wa Total wa Afrika ya Kati na Afrika Mashariki Bw. Jean Christian Bergeron na Mkurugenzi Mtendaji Total Tanzania Bw. Tarik Moufaddal.
Mhe. Rais Magufuli ameitaka Total kuharakisha ujenzi wa bomba hilo uliopangwa kuanza mwezi ujao na kukamilisha mapema hata kabla ya mwaka 2020 uliopangwa ili wananchi wa Tanzania na Uganda waanze kunufaika na mafuta hayo.
“Tuna matumaini makubwa na Total kuwa kazi hii mtaifanya haraka, na naomba niwahakikishie kuwa pamoja na soko la nje, kuna soko kubwa Afrika Mashariki yenye watu Milioni 165, na Serikali ya Tanzania itawapa ushirikiano wa kutosha wakati wote wa ujenzi na uendeshaji wa mradi ili mradi mnalipa kodi vizuri na mnazingatia sheria zetu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka kampuni hiyo kuzingatia kutoa ajira kwa Watanzania katika wilaya 24 ambazo bomba litapita huku akiwahakikishia kuwa Tanzania inao wakandarasi na wahandisi wa kutosha na wenye uwezo wa kushirikiana nao katika ujenzi wa bomba hilo.
Baada ya mazungumzo hayo Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bw. Charles Mwijage wamesema pamoja na kuja nchini kuangalia maandalizi ya ujenzi wa bomba, viongozi wa Total wameamua kuimarisha soko la mafuta Tanzania na pia kushirikiana na Serikali katika utafiti wa mafuta katika maeneo ya Ziwa Tanganyika, Eyasi Wembere na Ziwa Rukwa.
Kwa upande wake Bw. Momar Nguer amemshukuru Mhe. Rais Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni kwa msukumo mkubwa walioutoa katika kufanikisha mradi huu na ameahidi kuwa Total itahakikisha inakamilisha haraka mambo machache yaliyobaki ili kuanza ujenzi bila kuchelewa.
Bw. Momar Nguer amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake za kupambana na rushwa jambo lililosaidia kuimarisha mazingira ya uwekezaji na amemuhakikishia kuwa Total ipo tayari kufanya kazi bega kwa bega na Tanzania katika jukumu la utafiti wa mafuta katika maeneo yote yaliyotajwa.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) aliyemaliza muda wake Mhe. Abdulla Ibrahim Alsiwaidi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Abdulla Ibrahim Alsiwaidi kwa utumishi wake wa miaka 5 na amemuomba amfikishie salamu za shukrani kwa Rais wa UAE Mtukufu Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahyan kwa ushirikiano ambao Tanzania inaupata katika Nyanja mbalimbali za maendeleo na ustawi wa jamii.
Post a Comment