Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi ameumaliza mgogoro wa ardhi wa muda mrefu kati ya wakazi wa Mtaa wa Mtambani Vingunguti na mwekezaji wa kampuni ya PMM jijini Dar es salaam.
Mwekezaji huyo wa Kampuni ya PMM inayojihusisha na uhifadhi wa mizigo alitaka kuchukua eneo la hekari 228 lenye nyumba 4,000 na wakazi 70,000 wa Mtaa wa Mtambani Vingunguti.
Waziri Lukuvi amesema Serikali haitambui uwekezaji uliokuwa ufanyike na kwamba, mwekezaji hakufuata utaratibu uliyowekwa na Serikali, hivyo kusababisha mgogoro huo kuwa mkubwa.
Kwa mujibu wa wananchi wa eneo hilo tangu mwaka 2012 mwekezaji huyo aliwazuia kufanya shughuli zozote za uendelezaji kwa kile alichodai ameshafanya tathmini na anaisubiri Wizara ya Ardhi ambayo inamchelewesha, jambo ambalo Waziri Lukuvi amekanusha.
Mwekezaji huyo ametakiwa kurejesha nyaraka alizozichukua kwa wananchi hao kinyume na utaratibu na ametakiwa kuwalipa fidia wananchi kwakuwa aliwazuia wakazi hao kufanya shughuli zozote za uendelezaji kwa kile alichodai ameshafanya tathmini. Hata hivyo, hadi sasa hakuna kinachoendelea na malipo hayajafanyika.
Waziri lukuvi aliwaambia wananchi hao kuwa kuanzia leo haya maeneo ni mali ya wananchi kama anataka kununua aanze upya kufuata utaratibu uliowekwa, na haiwezekani mtu anakuja kuwanunua watu 70,000 kienyeji.
“Hatuzuii mtu kuuza mali yake, tunachosimamia sisi ni haki itendeke na utaratibu ufuatwe, lakini katika mchakato huu mambo yamekwenda ndivyo sivyo,” amesema Waziri Lukuvi.
Kwa upande wa meneja wa mradi wa PPM Bwana Deogratius Chacha amesema wapo katika hatua za mwisho na malipo yangefanyika ndani ya siku 90 zijazo ambapo wananchi hao hawakukubaliana na hilo.
Wakazi wa eneo hilo wamemwambia waziri Lukuvi kuwa mwekezaji amechukua pia leseni zao za makazi kwa muda mrefu na kushindwa kuendeleza makazi yao. Hata hivyo, hadi sasa hakuna kinachoendelea na malipo hayajafanyika zaidi ya ahadi na kwamba anasema Wizara ya Ardhi ndio inayomchelewesha.
Kauli hiyo imemfanya waziri Lukuvi kutoa agizo kwa meneja huyo kuwarudishia nyaraka zao wakazi wote hadi ifikapo kesho saa tano asubuhi. “OCD chukua vielelezo vya meneja, hakikisha hadi kufikia kesho saa tano awe amewarudishia wananchi nyaraka zao, kinyume cha hapo mkamate mweke ndani,” amesema waziri Lukuvi.
Na Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi
Post a Comment