*Na Shilatu E.J*
Lengo kuu la uanzishwaji wa chama cha kisiasa ni kukua na kuweza kushika dola. Tanzania ni nchi inayofuata mfumo wa vyama vingi na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema ni mojawapo ya chama cha kisiasa kilichotarajiwa na wengi kingeweza kuleta changamoto dhidi ya chama tawala CCM lakini ajabu yake imekuwa ndivyo sivyo.
Kadri siku zinavyozidi kusonga mbele ule umaarufu, sifa, msimamo, uhodari na umadhubuti wa ujenzi wa hoja unazidi kupungua siku hadi siku mpaka kufikia hatua wale waliokuwa wakikiamini chama cha Chadema kuanza kusema hakuna chama cha upinzani Tanzania. Wapinzani wote ni Watu wale wale.
Leo nitabainisha maeneo matatu ambayo yamepelekea kushuka kiwango, imani na sifa ya Chadema kwa jamii na wengi kusema Chadema wanafuata njia za kifo kama vilivyokufa vyama vya NCCR Mageuzi na CUF.
Mambo matatu yanayoonyesha anguko ni la Chadema ni:-
1. Kupatikana Mgombea wa Ukawa;
Kwa muda mrefu sana umaarufu wa Chadema ulitokana na namna ambavyo walivyojipambanua kupambana na ufisadi hapa nchini pasipo woga wala haya. Katika enzi ambazo Katibu Mkuu wa Chadema alikuwa Dk. Willbroad Slaa mapambano dhidi ya ufisadi yalikuwa yapo juu. Ikafika hatua mnamo Septemba 15, 2007 katika Viwanja vya Mwembe Yanga wakaweka historia ya kutaja kile walichokiita orodha ya Mafisadi nchini.
Walizunguka sehemu mbalimbali nchini kwa zaidi ya miaka 8 wakiwataja hao wanaowaamini ni Mafisadi. Jambo la kushangaza ndani ya dakika 5 mmojawapo wa wale aliokuwa akituhumiwa na Chadema kwa ufisadi alisimamishwa na Chadema hao hao kugombea urais kupitia mwavuli wa Ukawa! Watu wakabaki wakijiuliza Yule waliokuwa wakisema ni fisadi kwa zaidi ya miaka 8 iweje leo akumbatiwe na Chadema? Nani alimsafisha ufisadi wake mpaka wakaona ni mtu safi kwao? Kama walijua ni Mtu safi kwanini wazunguke nchi nzima kumchafua? Kama huyo aliekuwa mmojawapo ya watuhumiwa wamegundua ni Mtu safi, ina maana hata wale wengine waliotajwa nao pia walikuwa Watu safi pia?
Kwa kweli hakuna aliyeweza kuamini kipi kiliwabadilisha Makamanda wa Chadema kuamua kumkumbatia Yule waliyemtuhumu kuwa ni fisadi. Kitendo kile kiliwafanya Chadema waonekane sio Watu wa msimamo, ni Watu wazushi walioamua kupambana na ufisadi wakati wana punje ya ufisadi mdomoni.
2. UKUTA
Mnamo July 27, 2016 Chadema walizindua ‘Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (UKUTA) kama kitendo cha kupinga kile walichokiita ‘Matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia. Chama hicho kimetaja mambo 11 kinachodai kuwa yamefanywa na Serikali bila kufuata sheria na kanuni za nchi, likiwemo la kuzuiwa kwa shughuli za kisiasa na kutaja sababu 24 za kuibuka na Operesheni Ukuta.
Chadema wakapanga Septemba Mosi, 2016 siku ya kufanya mikutano nchi nzima kama ashilio la kupinga udkikteta nchini. Ajabu yake tarehe ilipofika kila Mtu ndani ya Chadema aliingia mitini na kutekeleza mpango wa kufanya mikutano nchi nzima ili kupinga udikteta.
Ukuta ukawa anguko la pili la Chadema kwa kushindwa mpaka kesho kuweza kufanikisha kufanya mikutano hiyo ya hadhara ya kupinga udikteta nchini. Wao wenyewe walisema wanafanya mikutano ili kupinga udikteta na wao wenyewe wakaja kuzuia kufanya mikutano hiyo! Ina maana kile walichodai ni udikteta kiliisha? Ama hapakuwa na udikteta bali ilikuwa gia ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa?
Kitendo cha Ukuta kufeli kulitoa jawabu la moja kwa moja la kutokuwa na kile walichokiita udikteta bali waliishia kupata aibu, fedheha na kusimangwa kila kona.
3. Mapambano ya Uchaguzi Huru na Haki.
Hivi karibuni vyama vinavyounda Ukawa viligoma kushiriki uchaguzi mdogo wa marudio wa Singida Kaskazini, Longido na Songea Mjini kwa madai ya kuanzisha mapambano ya uchaguzi huru na wa haki mpaka pale ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) watakapo kubali kukaa meza na Ukawa kujadili kero na Changamoto ili kuwe na uchaguzi huru wa haki. Kususa kwao hakukuzuia uchaguzi kufanyika.
Ajabu yake ilitokea pale ambapo NEC walipotangaza kufanyika uchaguzi mwingine mdogo wa majimbo ya Siha na Kinondoni utakaofanyika Februari 17, 2018 Ukawa wakiongozwa na Chadema wakatangaza nao pia kushiriki! Watu wakajiuliza ni lini Chadema na NEC waliketi kwenye meza ya mazungumzo? Madai yao na kero zao zimeshatatuliwa? Kama waliketi mrejesho wao upi? Ama NEC ile waliyokuwa wakiilalamikia imebadilishwa na sasa kuna nyingine?
Ni jambo la kustaajabisha kuona hakuna cha kikao, NEC kubadilishwa ama kero na madai yao kutatuliwa lakini Chadema wameamua kula matapishi yao kwa kushiriki uchaguzi wa Siha na Kinondoni na kutekeleza pembeni mapambano ya kudai uchaguzi huru na haki.
Chadema wamejionyesha sio chama sahihi cha mapambano dhidi ya ufisadi, mapambano ya kudai uchaguzi huru, mapambano ya kudai haki na demokrasia. Chama ambacho kimekosa msimamo, weledi wa kufanikisha maazimio yao, usaliti kwa Watanzania wa mara kwa mara hakifai.
Narudia kusema kurudi nyuma dhidi ya mapambano ya ufisadi, kupinga walichokiita “udikteta” na kushindwa kufanikisha azma ama ajenda ya kudai uchaguzi huru na haki unafanya Chadema kuwa chama cha hovyo na kisicho wafaa Watanzania.
*Na Shilatu E.J*
Januari 24, 2018
on Wednesday, January 24, 2018
Post a Comment