MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovic Utouh, amemuomba Rais John Magufuli kuendelea kusimamia suala la uwajibikaji kwa watumishi wote wa serikali kwa kuwa hatua alizozichukua zimesaidia kupunguza vitendo vya ufisadi.
Amesema vitendo hivyo vilikuwa vikifanywa na watu wachache kwa maslahi yao.
Utouh alitoa ombi hilo wakati akiwasilisha mada ya ‘uwajibikaji nguzo muhimu katika kuzuia rushwa’ katika mjadala wa wazi ulioandaliwa na Taasisi ya Wajibu na kuhudhuriwa na wahadhiri wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Utouh, ambaye pia ni mkurugenzi wa taasisi hiyo alisema kuwa, kazi inayofanywa na Rais Magufuli tangu aingie madarakani inastahili kuungwa mkono kwani amerudisha heshima, nidhamu na wajibu kwa kila mtumishi kuheshimu nafasi aliyo nayo pamoja na kupunguza vitendo vya rushwa.
Alisema kuwa kabla ya Rais Magufuli kurudisha nidhamu katika utawala wake, wapo baadhi ya watumishi waliokuwa wakifanya vitendo vya kifisadi pasipo kuzingatia sheria za nchini, hali ambayo ilikuwa ikiumiza zaidi wananchi wa hali ya chini na kumuomba kuongeza kasi hiyo ili kumaliza vitendo hivyo.
Mkurugenzi wa sera kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Sabena Seja, alisema uwajibikaji kwa watumishi wa umma umeongezeka kutokana na hatua kuchukuliwa na kuongeza kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanapaswa kuongezewa nguvu kwa kuwa bado rushwa inawaathiri wananchi.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prof. Gauka Nyamsogoro, alipongeza Taasisi ya Wajibu kwa kuendesha mijadala ya wazi inayoongeza tija na kuandaa kundi la vijana ambao watakuwa na uzalendo katika miaka ijayo ambao baadhi yao watakuwa viongozi.
Awali Meneja Utafiti na Programu wa taasisi hiyo, Moses Kimaro, alisema wamelenga kustawisha uwajibikaji kwa makundi ya vijana katika vyuo vikuu vyote nchini ili kuwa na uzalendo.
Alisema mjadala huo ni sehemu ya uzinduzi wa mijadala mingine itakayofanyika katika vyuo vikuu kuelezea juu ya ubaya wa rushwa na kuwa na wahitimu watakaopambana na kuchukia rushwa na kuwajibika.
Akizindua mjadala huo, Mkurugenzi wa Sera na Utawala Bora katika Ofisi ya Rais, Mathias Kabundunguru, alisema mijadala hiyo ni sehemu ya mustakabali wa kujenga uchumi kwa faida ya nchi kwani inasaidia kuongeza uelewa kwa Watanzania hasa katika uchumi wa kuelekea viwanda.
on Monday, January 29, 2018
Post a Comment