Subira Kaswaga – NEC
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa uchaguzi mdogo katika majimbo ya Siha mkoani Kilimanjaro na Kinondoni mkoani Dar es Salaam pamoja na Kata nne za Tanzania Bara utafanyika Februari 17, 2018 kufutia waliokuwa Wabunge katika majimbo hayo kujivua Uanachama na kukosa sifa za kuendelea kuwa wabunge.
Taarifa ya Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Hamid Mahmod Hamid imeeleza kuwa pamoja na Majimbo hayo,pia Kata nne za Isamilo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Manzase Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Madanga Halmashauri ya Wilaya ya Pangani mkoani Tanga na Kimagai Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma zitafanya Uchaguzi mdogo
Aidha, Jaji Mkuu (Mst. Zanzibar) Hamid Mahmoud Hamid amesema kuwa, Tume inaendesha uchaguzi huo baada ya kupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mh. Job Ndugai kuhusu uwepo wazi wa jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam na Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro.
Jaji Mahmoud amesema kuwa, barua hiyo ilieleza kuwa majimbo hayo yapo wazi baada Maulid Mtulia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kujivua uanachama wa CUF na Dr. Godwin Mollel wa jimbo la Siha kujiuzulu uanachama wa CHADEMA na hivyo wote kukosa sifa za kuwa Wabunge.
Pia, ameeleza kuwa Tume ilipokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa ikiitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Udiwani katika kata nne za Tanzania Bara.
“Baada ya kupokea barua hizo Tume kwa kuzingatia vifungu vya 37(1) na 46(2) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 pamoja na kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa sura ya 292 inatangaza kuwa majimbo mawili na kata nne zipo wazi” alisema Jaji Mahmoud.
Ameeleza kuwa, fomu za uteuzi kwa majimbo hayo mawili na kata nne itakuwa kati ya tarehe 14 – 20 Januari, 2018, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 20/01/2018, na Kampeni za uchaguzi mdogo zitafanyika kuanzia tarehe 21/01 – 16/02/2018 na siku ya uchaguzi itakuwa tarehe 17/02/2017.
Vilevile, Jaji Mahmoud amevikumbusha Vyama vya Siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo yote wakati wa uchaguzi huo mdogo.
Post a Comment