Na Emmanuel J. Shilatu
Tofauti na mataifa mengine Watanzania wako huru zaidi kwenda kokote kule ndani ya nchi na hata kuishi au kufanya kazi ama biashara bila ya bughudha yoyote endapo taratibu na sheria zitazingatiwa vyema.
Hali hii ni tofauti na nchi nyingine zikiwemo za jirani kama vile Kenya, Kenya Rwanda, Burundi, Kongo na hata Uganda ambapo ukabila umetalaki kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa lakini kwa Tanzania hakuna ubaguzi wa rangi,dini wala kabila.
Hiyo inatokana na uongozi imara, sera safi, upendo na kila aina ya ubora uliotukuka ndani yake kwa jamii ya kitanzania. Jambo linaloendelea kutia faraja ni kuwa tangu ianzishwe CCM toka zao la TANU na ASP imeendelea kuwa ni chama kinachotawala na kuongoza nchi. Na siri yote ya mafanikio hayo ni kutokana na kuwa nguzo imara ambazo ni Wanachama, Ilani ya chama, na Viongozi wake.
Wanachama wake ambao ndio mtaji wa chama wapatao zaidi ya milioni 12 na mashabiki wapatao ama zaidi ya milioni 16. CCM ni chama kisichozingatia uwepo au hata harufu ya ubaguzi wa rangi, kabila au dini ya mtu.
Hatua hio imewafanya Watanzania wengi kuanzia vijana kwa wazee, wake kwa wanaume kujivunia kuwa wanachama makini wa chama chenye mtazamo chanya wa kuwavusha kwenye neema. Ili kuhakikisha CCM inapata makada wa aina tofauti bila ya kujali umri, jinsia ilianzisha jumuiya za wazazi, wanawake (UWT) na vijana (UVCCM) ambazo ni viungo muhimu vya chama katika kuwaweka watu wote pamoja na karibu na hivyo kuendelea kuwa chama cha kishujaa katika kuwakomboa watu wake.
Pia kuna suala zima la uwepo wa ilani ya uchaguzi ambayo ni mkataba baina ya chama na wananchi au viongozi na wananchi ambao ndio wapiga kura wenyewe kupitia ilani, CCM inatoa ahadi zake mbalimbali za kutekelezwa katika muda uliopangwa wa miaka mitano.
Ni wazi kwamba ahadi hizo zimekuwa zikitekelezwa kwa kiwango kikubwa na cha kuridhisha kiasi cha kufanya Watanzania waendelee kuwa na imani nayo kila uchaguzi unapowadia. Hii inajidhihirisha wazi katika chaguzi kuu mbalimbali zilizofanyika mara tatu 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015 ambapo CCM iliibuka na ushindi wa kishindo.
Nguzo nyingine kuu ya CCM ni viongozi wake. Ndani ya CCM wenye dhamana ya chama ni wanachama wenyewe na wala si viongozi. Hali hii imesaidia kutokuwa na hata chembe au harufu ya umini wa mtu kujiona kuwa ana haki miliki ndani ya chama au ni kiongozi wa maisha. Ikumbukwe kuwa CCM ina haki zote kwa kiongozi yeyote yule aliyetokana na CCM.
Hiyo ni ishara kwamba ni chama chenye misingi imara ya uongozi na ndio maana kumekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi kwa kufuata misingi ya katiba ya chama. Kila baada ya mitano hufanyika uchaguzi wa viongozi wa mashina hadi Taifa na katika uchaguzi huo ndipo watu huingia na kutoka.
Aidha hali hii ni tofauti na vyama vingine nchini ambavyo walivyoviasisi ni viongozi wa kudumu hadi hii leo. Wanapoambia kuna uchaguzi baadhi ya viongozi hao kufanya mizengwe kwa wale wanaonyesha nia ya kuleta mabadiliko na hata kuwafukuza.
Kwa sasa CCM ipo chini ya Uenyekiti wa Rais Dk. John Pombe Magufuli ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inaendelea kuongoza kupitia ridhaa ya Wananchi.
Ridhaa hii inatokana na CCM kuendelea kuwa na uongozi imara, sera safi, maendeleo bora na hivyo kuendelea kuwa tegemeo la kila Mtanzania anayependa haki na maendeleo pamoja na ustawi uliopo.
Nyakati zote CCM imeendelea kuwa mstari wa mbele kwenye mapambano dhidi ya maadui wakuu watatu ujinga, maradhi na umaskini hali iliyopelekea maendeleo makubwa chanya nchini. Kama haitoshi Rais Dk. Magufuli ameonyesha umahiri na uzalendo wa hali ya juu wa kulinda rasilimali zetu mathalani madini na kuweka uwazi juu ya madini.
Katika idara ya ubadhilifu wa mali za umma nako harakati za mapambano hazikuwa nyuma. Tumeshuhudia idara mbalimbali zikibanwa mbavu kwa uthibiti imara kabisa tofauti na mitazamo hasi ya baadhi ya watu yalivyo. Mifano husika ni katika idara za maliasili, uvuvi, bandari, madini, chakula ambapo kote kumekuwa na uthibiti tulioshuhudia wa mapato na rasilimali za Watanzania.
CCM hii hii imekuwa mstari wa mbele kupambana na mafisadi (hawa ni wahujumu uchumi wanaotafuna rasilimali na mali za umma) Serikali za CCM imeweza kuvipa nguvu idara za kisheria ili kuweza kupambana na aina yeyote ilaya ubadhilifu na uhujumu uchumi. Kwa kutambua mgawanyo wa mihimili ya madaraka vimeachiliwa vyombo husika kufuatilia ili haki ipatikane bila kuhujumu upande wowote. Huu ndio utawala wa kisheria.
Mbali na hayo yapo mambo mengi ambayo CCM imefanya mapinduzi zaidi kupitia sera na ilani ambazo zipo kwa ajili ya kumlinda, kumtetea na kumkomboa mtu wa tabaka la chini na kati ambao ndio , asilimia kubwa ya Watanzania.
CCM inaundwa na Wanadamu ambapo inafahamika vyema kuwa Binadamu si Malaika hajakamilika na kwa kuwa CCM ipo kama Mwanadamu nayo pia haijakamilika, kuna sehemu imefanya vizuri sana, kuna sehemu imefanya vizuri na kuna sehemu pia haijafanya vizuri. CCM kama chama cha kisiasa chchote kile Duniani hakitaweza kumridhisha kila Mtu kwa kiwango kile anachotarajia.
Lakini hali hiyo haitaweza kufuta mazuri ambayo CCM kupitia serikali zake zilizokuwa na iliyopo madarakani kujivunia mafanikio yaliyopatikana toka enzi za kulikomboa Taifa letu toka kwa wakoloni Waingereza mpaka hapa ilipoifikisha.
Wakati CCM ikiadhimisha miaka 41 ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake haina budi kubadilika na kuendana na kasi ya Mwenyekiti wake Rais Magufuli, kuendana na kasi ya Hapa Kazi Tu. Tuendelee kuthamini na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dk. Magufuli anayeleta mageuzi ya kiuchumi nchini.
Heri ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi!
Na Emmanuel J. Shilatu


Post a Comment