Serikali imesema itaongeza mishahara ya watumishi wa umma mwaka ujao wa fedha. Pia imesema hadi kufikia Jumamosi itakuwa imetoa ajira mpya 22,150 kwa mwaka huu wa fedha.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jijini Dodoma jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, alipokuwa anachangia mjadala wa mapendekezo ya bajeti kuu ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha na Taarifa ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017.
Alisema serikali ilisimamisha utoaji ajira, ili kuhakikisha uhakiki wa wafanyakazi hewa unafanyika lakini baada ya zoezi hilo kukamilika sasa, ajira zimeshaanza kutolewa.
Mkuchika alisema uhakiki huo ulibaini watumishi hewa 19,708 na wengine 14,409 walio na vyeti feki.
Alisema kuwa hadi Jumamosi ajira 22,150 zitakuwa zimetolewa. Kati yake 7,000 ni za walimu na 8,000 za kada ya afya.
Hata hivyo, lengo la serikali mwaka huu wa fedha lilikuwa kuajiri watumishi wapya 52,000.
"Waheshimiwa wabunge kwa ajira hizo, hakuna zahanati itakamilika halafu ikakosa watumishi," Mkuchika alisema.
Kuhusu watumishi wa umma kutopandishwa mishahara kwa muda mrefu, Mkuchika alisema hoja hiyo si sahihi kwa kuwa serikali imeshatoa nyongeza ya mwaka 2017/18 na katika mwaka ujao wa fedha 2018/19 itatolewa.
Hata hivyo, waziri huyo alibainisha kuwa sasa serikali inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ukiwamo utoaji huduma za afya na maji itakayowezesha kuimarisha uchumi wa nchi.
Alisema kuwa mara uwezo wa kibajeti ukiwa mzuri serikali haitosita kupandisha mishahara kwa watumishi wa umma.
"Kwa watumishi ambao walipaswa kupandishwa madaraja, lakini hawakupata fursa hiyo hadi wakastaafu, wanapaswa kwenda kwa waajiri wao wajaziwe fomu maalum ili walipwe malipo yao," Mkuchika alisema.
Post a Comment