Ukamataji huo umekuja baada ya kuibuka wimbi la walaghai ambao hutuma jumbe mbalimbali kwa watu zinazoshawishi kutuma fedha au kufanya malipo ya kifedha kwa njia ya simu pesa.
Kutokana na wimbi hilo la matapeli kuongezeka, mapema mwezi huu Jeshi la Polisi lilitahadharisha wananchi kuzipuuza jumbe hizo na kuwataka waliotapeliwa kupitia 'SMS' hizo kutoa taarifa kituo cha polisi kilicho karibu yao.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Liberatus Sabas, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa watuhumiwa hao 15 wamekamatwa katika operesheni maalum.
Alisema walikutwa na laini za simu 352 za mitandao mbalimbali zenye usajili usio na utambulisho wa watuhumiwa hao.
Pia, Kamanda Sabas alisema, matapeli hao wamekutwa na vitambulisho mbalimbali 31 vikiwa pamoja na leseni, kadi za benki, kompyuta mpakato tano, kompyuta moja na modemu mbili.
“Watu hawa wamekiri kutumia mfumo wa simu inayoitwa 'Bulk SMS' (SMS za mkupuo), ambayo ina uwezo wa kutuma jumbe fupi zaidi ya 10,000 kwa siku na inazalisha namba nyingine za kupokea ujumbe baada ya kuweka namba ya kwanza,” alisema.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa kwa ushirikiano wa mkoa wake, mikoa ya jirani na Rukwa.
Kamanda Sabas alimtaja mmoja wa watuhumiwa hao kuwa ni Lule Lusale (35), mkazi wa Eden Ng’ambo mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.
Alisema ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakidai kupokea jumbe hizo.
“Katika kipindi cha kuanzia mwezi Aprili 2018 kumekuwa na jumbe fupi za maneno ambazo zimekuwa zikitumwa kwa watu mbalimbali zenye maneno ‘Nitumie hiyo hela katika namba hii... namba ile ya awali ina matatizo; nitumie sasa hivi,” alisema Sabas.
Kamanda Sabas alitaja baadhi ya namba ambazo matapeli hao walikuwa wakizitumia kutuma jumbe hizo za kitapeli kuwa ni 0758713746, 0764581220, 0744105579.
Alisema uchunguzi zaidi unaendelea na pindi utakapokamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.
Post a Comment