Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (katikati), akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara yake aliyoifanya leo Julai 5, 2018 kutembelea mradi wa uboreshaji wa mfumo wa usambazaji maji Dar es Salaam na Pwani (kushoto) ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA), Dkt. Suphiani Masasi na kulia ni Mkandarasi wa mradi huo kutoka kampuni ya Jain Irrigation ya nchini India, Bw.Anil Vitankar.
NA K-VIS BLOG/Khalfan Said
WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, leo Julai 5, 2018 ametembelea mradi wa uboreshaji wa mfumo wa usambazaji maji Dar es Salaam na Pwani ambao umefikia asilimia 87.5 na kumuhimiza mkandarasi kumalizia asilimia iliyobaki kwa wakati vinginevyo atachukua hatua kali
Profesa Mbarawa alisema, mradi huo ambao unatekelezwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Mai Safi na Maji Taka (DAWASA), unathamani ya shilingi bilioni 72.43 na ni mradi muhimu sana katika utoaji huduma kwa wananchi.
“Mkandarasi yuko kwenye site lakini kasi yake hairidhishi, hivyo sisi kama serikali tunajaribu kutatua kero hii ya maji kwa wananchi, lakini mkandarasi kidogo analeta shida, kama mjuavyo mradi ulianza mwaka 2016 mwezi Machi na ulitarajiwa kukamilika Novemba 2017 utaona tuko nyuma karibu miezi 18 tuko nyuma.” Alisema na kutoa maelekezo
“Kwanza tunataka uwepo kwenye site saa 24, na sio tunakuona tu lakini tuone unafanya kazi, pili ukishinbdwa kumaliza mradi huu kama tulivyokubaliana mwezi Septemba uelewe kwamba hii ndio itakuwa mara yako ya mwanzo na ya mwisho kupata kazi tena hapa Tanzania, na tatu tutakutoa kwenye usajili wa chama cha makandarasi yaani bodi ya makandarasi nah ii maana yake hutaweza kufanya kazi tena hapa Tanzania na mwisho tutachukua Pasipoti yako ya kusafiria ili kuhakikisha kwamba unafanya kazi na unamaliza.” Alisema.
Ziara hiyo ya Profesa Mbarawa imemuwezsha kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo ulioanza Machi 2016 na unaohusisha ujenzi wa matenki matano (5) ya kuhifadhi na kusambaza maji yenye ukubwa wa kuhifadhi lita milioni 5.0 hadi 6.0.
Pia alitembelea ujenzi wa vituo vine (4) vya kusukuma maji vilivyo na matenki yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 3.0 kila moja, ununuzi na ufungaji wa pampu kubwa 16 za kusukuma maji ununuzi wa transfoma na ufungaji wa njia za umeme wa msongo mkubwa, ununuzi na ulazaji wa mabomba makubwa ya ugawaji maji na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji mitaani yatakayokuwa na urefu wa jumla ya kilomita zipatazo 477.
Kwa mujibu wa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Dkt. Suphiani Masasi, mradi huo utanufaisha maeneo ya Salasala, Bunju, Wazo, Makongo, Changanyikeni, Bagamoyo, Mpiji, Zinga, Kiromo, Kitopeni, Ukuni, Kerege, Buma, Mataya na ukanda maalum wa WPZA ambayo ni maeneo yanayohudumiwa na mtambo wa Ruvu Chini.
Aidha mradi pia utanufaisha maeneo yaliyopo kati ya Mbezi Louis na Kiluvya ambayo ni Kiluvya yenyewe, Kibamba, Mbezi, Msakuzi, Makabe, Malamba- mawili na Msigani na maeneo haya yanapata maji kutoka Mtambo wa Ruvu Juu ambao ulizinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanania Juni 2, 2017.
Mtendaji Mkuu huyo wa DAWASA alimueleza Mhe. Waziri kuwa lengo la mradi ni pamoja na kuhakikisha kuwa wananchi wa kawaida wenye viwanda na biashara katika eneo lote la mradi wanapata huduma bora za maji hasa baada ya maji kuongezeka kufuatia kukamilika kwa kazi za upanuzi wa mitambo ya maji Ruvu Juu na Ruvu Chini.
Muonekano wa sasa wa tanki kubwa la kuhifadhia maji e neo la Changanyikeni jijini Dar es Salaam ambapo tayari tenki hilo limeshafunikwa.
Muonekano wa kituo cha kusukuma maji cha Salasala
Huu ni muonekano wa Tanki la kuhifadhia maji la Changanyikeni jijini Dar es Salaam.
Profesa Mbarawa, akiongozana na Bi.Modester Mushi (kulia), ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa ufundi DAWASA, wakati Mhe. Waziri alipotembelea eneo la ujenzi wa kituo cha kusukuma maji cha Boko ambacho ujenzi wake umefikia hatua za mwisho.
Profesa Mbarawa akitoa maagizo hayo.
Bw. Anil Vitankar, wa kampuni iliyopewa kandarasi ya ujenzi wa mradi huo ya Jain Irrigation, akisikiliza maagizo ya Mhe. Waziri.
Baadhi ya vifaa vya kukamilisha mradi huo vikiwa kwenye karakana huko Boko nje kidogo ya jiji
Post a Comment