Na Mahmoud
Zubeiry
KOCHA
Muingereza Stewart Hall amerejea na ‘bonge la zali’, baada ya leo kuiongoza timu
hiyo kuichapa Coastal Union ya Tanga mabao 4-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje
kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Stewart
alitua jana usiku Dar es Salaam akitokea Kenya alipokuwa anaifundisha Sofapaka
ya Ligi Kuu ya huko, baada ya kufukuzwa Azam Agosti mwaka huu na leo ameanza
kazi, akirithi mikoba ya Mserbia, Boris Bunjak aliyefukuzwa
Jumatatu.
Kwa ushindi
huo, Azam imefikisha pointi 21, baada ya kucheza mechi 10 na sasa inarejea
nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Simba na Yanga, zenye pointi
23 zote baada ya kucheza mechi 11, kila timu.
Katika mechi
hiyo iliyochezeshwa na refa Simon Mbelwa, aliyesaidiwa na Abdallah Rashid wote
wa Pwani na Michael Mkongwa wa Njombe, hadi mapumziko Azam tayari walikuwa
wanaongoza kwa mabao 3-0.
Gaudence
Mwaikimba aliifungia Azam bao la kwanza kwa kichwa dakika ya 23 kabla ya Kipre
Tcheche kufunga la pili dakika ya 36, baada ya kuipasua ngome ya Coastal na
Khamis Mcha ‘Vialli’ akafunga la tatu dakika ya
44.
Coatsal
walianza vizuri mechi hiyo na kusukuma mashambulizi langoni mwa Azam, lakini
baada ya dakika 20, wakapoteza mwelekeo na kuanza kuwaruhusu wapinzani wao
kuvuna mabao.
Kipindi cha
pil, Azam walirudi na moto wao, lakini kidogo Coastal walibadlika nao na kufanya
mchezo uwe mgumu kidogo.
Hata hivyo,
walikuwa ni Azam tena waliotikisa nyavu za Coastal, baada ya kiungo Othman Tamim
kujifunga dakika ya 73 katika harakati za kuokoa.
Baada ya bao
hilo, Coastal walizinduka na kuanza kushambulia kupitia pembeni, jambo ambalo
liliwasaidia kupata bao la kufutia machozi lililofungwa ma kiungo Jerry
Santo.
Kwa ujumla
katika mchezo wa leo, Coastal walizidiwa katika safu ya kiungo ambako leo
Stewart alipanga viungo wengi waliotekeleza majukumu yao
vyema.
Baada ya
mchezo huo, kocha wa Coastal, Hemed Morocco alisema kwamba walizidiwa uwezo na
wapinzani wao na kwa ujumla vijana wake walicheza chini ya kiwango leo, hata
hivyo anakwenda kufanyia kazi makosa ili timu irejeshe makali
yake.
Stewart
alisema anafurahi kukaribishwa na ushindi huo mnono na kwamba hizo ni dalili
njema. Aliwapongeza vijana wake kwa kucheza kwa kufuata maelekezo yake na
akasema kwamba sasa anaelekeza nguvu zake katika mchezo ujao dhidi ya Yanga
Jumapili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Azam FC; Mwadini Ally, Samir Hajji, Ibrahim Shikanda, Aggrey
Morris, Said Mourad, Kipre Balou/Ibrahim Mwaipopo, Jabir Aziz, Salum
Abubakar/Himid Mao, Gaudence Mwaikimba/Abdi Kassim, Kipre Tcheche na Khamis Mcha
‘Vialli’.
Coastal
Union; Jackson
Chove, Said Swedi, Juma Jabu, Mbwana Hamisi, Jamal Machelanga/Salim Gilla, Jerry
Santo, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Razack Khalfan/Hamisi Shango, Daniel Lyanga,
Atupele Green/Lameck Dayton na Othman Tamim



Post a Comment