Rais Mstaafu wa Msumbiji 'Joaquim Chisano. |
BAADA ya mvutano wa muda mrefu hatimaye Serikali za Tanzania na Malawi zimekubaliana kupeleka
mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa katika jopo la viongozi wastaafu wanaoshughulikia migogoro ya nchi mbalimbali
barani Afrika.
Hatua hiyo imekuja baada ya pande hizo mbili kushindwa
kuafikiana katika mazungumzo yaliyomalizika jana jijini Dar es Salaam,
yaliyowakutanisha mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo mbili sambamba na
viongozi mbalimbali wa serikali za nchi hizo.
Uamuzi huo umekuja siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuwaeleza waandishi wa habari
kwamba Ziwa Nyasa ni urithi wa nchi tatu Tanzania, Malawi na Msumbiji na hivyo
siyo sahihi upande wowote kati ya nchi hizo kudai unamiliki sehemu kubwa ya
ziwa.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo, Membe
pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Muganda Chiume alisema viongozi hao
wastaafu watasaidia kumaliza tatizo hilo.
Membe alisema mapendekezo ya mazungumzo hayo yatapelekwa
kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Malawi, Joyce Banda, wao watapeleka barua
katika jopo hilo.
“Mazungumzo yetu naweza kusema tumekubaliana na pia
hatujakubaliana, hivyo tumeamua kwenda katika hatua nyingine ya usuluhishi
ambayo ni kwa jopo la viongozi wastaafu
linaloongozwa na Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano,” alisema
Membe na kuongeza:
“Nitapeleka barua hiyo Machi 24 mwakani na endapo jopo hili
litashindwa kufikia mwafaka tutaangalia uwezekano wa kwenda katika Mahakama ya
Kimataifa ya Haki (ICJ).”
Membe alifafanua kuwa Serikali ya Tanzania inaweza
kuipeleka Serikali ya Malawi ICJ, lakini Malawi haiwezi kuipeleka Tanzania
katika mahakama hiyo kutokana na kuwa nchi hiyo haikusaini makubaliano ya
lazima.
Kwa upande wake Chiume alisema kuwa uamuzi utakaotolewa na
jopo hilo wataukubali kwa kuwa wanaliamini katika utendaji wake wa kazi.
Alisema kuwa Malawi ilifurahishwa na kauli ya Rais Kikwete
wakati akizungumza katika mkutano mkuu wa CCM uliomalizika hivi karibuni mjini
Dodoma kwamba, nchi hizo mbili hazitaingia vitani.
“Kikwete na Banda wote kwa pamoja wamekuwa wakitoa kauli
nzuri ambazo zinaonyesha kuwa nchi hizi mbili hazitaingia vitani kitu ambacho ni
kizuri,” alisema Chiume.
Mgororo ulivyoanza
Mgogoro huo ulianza Julai mwaka huu baada ya Malawi kuanza
kufanya utafiti wa mafuta katika eneo la Tanzania, hali ambayo ilisababisha
serikali hizo mbili kuanza kulumbana.
Serikali ya Tanzania ilipiga marufuku ndege za utafiti wa
mafuta za Malawi kuruka katika anga ya Tanzania.
Source: Mwananchi
Post a Comment