SEKRETARIETI mpya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
iliyoingia madarakani hivi karibuni chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete,
imesema itahakikisha vitendo vya rushwa hasa kwenye chaguzi za chama hicho
vinakoma mara moja, tofauti na ilivyokuwa imezoeleka.
Kauli hiyo
ya viongozi wa juu wa CCM, Mwenyekiti Taifa (Rais Kikwete), Makamu Mwenyekiti
Tanzania Bara (Phillip Mangula) na Katibu Mkuu (Abdulrahman Kinana) imetolewa
jana na viongozi hao wakati wakizungumza na wana-CCM Mkoa wa Dar es Salaam
katika mkutano wa kumpongeza Rais Kikwete kuchaguliwa kushika nafasi hiyo
tena.
Akizungumza
na umati wa wanachama hao, Rais Kikwete aliwataka viongozi wapya kufanya kazi ya
ziada ya kuhakikisha wanarejesha imani ya Watanzania kwa CCM, ambayo haiko kama
ilivyokuwa zamani. “Lazima kujiuliza nini kimekifanya chama hiki kufikia hapo
kilipo na kuangalia nini cha kufanya ili kuondokana na hali hiyo. Pale mnapohisi
hali ya kuungwa mkono inapungua lazima tujiulize, kulikoni..! Nini cha kufanya
ili kuimarisha chama,” alisema na kuongeza kuwa kazi nyingine ni kuhakikisha
wanakijenga chama na kuimarisha zaidi ili kiendelee kuwaongoza
Watanzania.
“Chama
chetu hakifanyi mikutano…wenzetu wanafanya kwanini sisi hatufanyi, sasa
tutatengeneza utaratibu maalumu kuhakikisha viongozi wa chama kwa nafasi zao
wanafanya kazi yao ipasavyo ndani na nje ya chama,” alisema Rais
Kikwete. Alisema ipo haja ya kujipanga na kuangalia namna ya kupambana na
propaganda hasi za baadhi ya vyombo vya habari na wapinzani ili kukabiliana na
hali hiyo. Aliwataka wanaCCM kuacha makundi na chuki ambayo yamekuwa yakikigawa
chama hicho.
Awali
akizungumza Kinana alisema vitendo vya rushwa ndani ya CCM watahakikisha
vinakoma mara moja ili kurejesha imani ya Watanzania iliyopungua kutokana na
tuhuma za wachache dhidi ya vitendo viovu. Alisema chini ya uongozi wake
atahakikisha mashaka yaliotawala kwa wananchi dhidi ya CCM yanaondoka kwa
kuwaengua wale wanaoendeleza vitendo vya rushwa, majumbu na vitendo vinavyo leta
sifa mbaya ya chama hicho.
“Hatuwezi
kuiongoza nchi yetu wakati watu wanamashaka na sisi, lazima tuondoe mashaka
akisimama mwana-CCM wote waseme naam huyu anaweza kusema…sio akisimama mwana-CCM
kusema watu wanahoji haaah, na huyu naye anakemea rushwa? Aliwataka wana-CCM
kushirikiana katika kukisafisha chama na si kuwaachia viongozi jukumu hilo,
ambalo wao kama viongozi wamekubali kuongoza mapambano hayo.
Post a Comment