![]()  | 
| Kutoka kulia peomota anayemleta JB, GuyGuy Kiangala, Chaz Baba, Muhonda na Dodo | 
Na Mahmoud 
Zubeiry
MWANAMUZIKI 
nguli wa dansi Afrika, JB Mpiana anatarajiwa kuwasili nchini Novemba 26, mwaka 
huu kwa ajili ya kupamba uzinduzi wa albamu ya Mashujaa Band Novemba 30, mwaka 
huu katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam na baadaye katika mikoa ya 
Arusha Novemba 28 na Mwanza Desemba 2.
Akizungumza 
na Waandishi wa Habari asubuhi ya leo katika ukumbi wa Millennium Business Park, 
Kijitonyama, Dar es Salaam, rais wa bendi ya Mashujaa, Charles Gabriel Cyprian 
‘Chaz Baba’, alisema mkali huyo wa dansi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo 
(DRC) anakuja kundi lake zima la Wenge Musica 
BCBG.
JB Mpiana 
ambaye kwa sasa anatamba na albamu yake ya mpya iitwayo Biloko, anatarajiwa 
kupagawisha Watanzania na rap yake mpya iitwayo Amataka Na Punda yaani, Panda 
Punda, ambayo kwa Kongo inapendwa ile mbaya.
Chaz Baba 
alisema kwamba maandalizi ya onyesho lao yanaendela vizuri kwa ujumla na 
wanamuziki wapo tayari kuwapa raha Watanzania siku 
hiyo.
Chaz Baba 
alisema bendi yao itaingia kambini wiki ijayo nje kidogo ya Dar es Salaam, 
ambako hawataki kuweka wazi, ili kuwaepushia usumbufu wanamuziki wakati zoezi 
hilo gumu la maandalizi ya shoo ya kufa mtu.
Alisema 
albamu yao, wanayozindua iitwayo Risasi Kidole ina nyimbo sita, ambazo ni 
Risasi Kidole yenyewe utunzi wake Chaz Baba, Ungenieleza utunzi 
wake Raja Ladha, Umeninyima utunzi wa Freddy Masimango, Hukumu ya 
Mnafiki utunzi wake Jado FFU, Kwa Mkweo utunzi wake Baba Isaya na 
Penzi la Mvutano, ambao umetungwa na Masoud Namba ya 
Mwisho.
Chaz Baba 
alisema kama ilivyopangwa, mbali na JB Mpiana, wanamuziki wengine watakaopamba 
uzinduzi huo ni MB Dogg, H Baba, Ney wa Mitego na wengineo ambao watajulikana 
baadaye.
“Sisi kwa 
upande wetu tumejipanga vizuri kuwapa watu burudani ambayo tunajua kwa muda 
mrefu wameikosa, Mashujaa tunakuja kushujaa, ushujaa wa kuwaburudisha watu na 
kukata kabisa kiu yao,”alisema Chaz Baba.
Alisema 
wanataka kufanya shoo ambayo hata JB mwenyewe akiona atakubali kwamba Tanzania 
kuna bendi yenye ubora sawa na bendi za kwao, Kongo, ambayo ni 
Mashujaa.
“Hadi sasa 
wapenzi wa muziki hapa Dar es Salaam ambao wamebahatika kuona shoo zetu wanakiri 
sisi ndio mabingwa wapya wa muziki wa dansi Tanzania, sasa tunataka 
tumdhihirishie hilo na JB Mpiana,”alisema Chaz 
Baba.
Wakati 
onyesho la Dar es Salaam litafanyila Leaders, Mwanza itakuwa kwenye ukumbi wa 
Villa Park na Arusha ni Tripple A.




Post a Comment