MKUU WA MKOA
Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi amewataka wanafunzi wa vyuo vya
elimu ya juu walioko katika mkoa huo kujihoji
nafsi zao na kucheki matendo yao kama kweli ni ya kumpendeza Mungu kwa vile
ndiyo yanachangia wao kutotambua umuhimu wa nafasi
walizonazo.
Dk. Nchimbi ametoa kauli hiyo
mwishoni mwa wiki wakati akihutubia maelfu ya wanavyuo waliohudhuria Jumuiko la
Wanavyuo wa Dodoma (Dodoma Campus Night) lililoambatana na mkesha wa
kusifu na kuabudu uliofanyika kwenye ukumbi wa Chimwaga mjini
Dodoma.
Jumuiko hilo lilihudhuriwa na wanafunzi
zaidi ya 3,500 wa dini mbalimbali kutoka vyuo vikuu vya Dodoma (UDOM), St.
John’s, Vyuo vya Mipango, Madini, Mirembe, Hombolo, Chuo cha Elimu ya Biashara
(CBE) na vyuo vya ualimu vya Mitumba na Capital.
Dk. Nchimbi alisema wanavyuo wengi ambao
walifaulu kidato cha sita kwa alama za juu (first class) huwa wanaporomoka
kimasomo wanapoingia kwenye vyuo vya elimu ya juu kwa sababu hawajiweki sawa
kwenye mahusiano yao na Mungu aliyewaumba. “Wanaharibikiwa kwa sababu hawajiweki
sawa na Mungu… hawakai pale ambapo Mungu anataka wawe (their right position),”
alisema.
“Tunzeni nafasi zenu ambazo Mungu
amewapatia… uwingi wenu huu katika usiku wa leo hauna maana kama hatutakuwa na
uhusiano mwema na Mungu kwani hata shetani ana watu wake na huwa anawapatia
mahitaji yote… kila mmoja wenu aanze upya na Mungu”,
alisema.
“Tumfikirie Mungu, tuangalie mahusiano yetu
na Mungu wetu yakoje na tumuombe atusaidie katika yote tuyatendayo, naye
atatujibu kwa sababu Mungu huwa hawekezi kwa hasara bali huwekeza kwa faida,”
alisema huku akishangiliwa na wanafunzi waliokuwa wamefurika kwenye ukumbi
huo.
Alisema idadi kubwa ya wanavyuo wakishapata
fedha za mkopo hutumbua maisha kwenye vilabu vya muziki ambavyo ni maarufu mjini
humo kama vile Club 84, Club La Aziz na Maisha Club na hawarudi vyuoni hadi
fedha yote imekwisha.
“Mungu alipofanya uumbaji alisema kila
alichokifanya ni chema sana. Sasa kama wewe ni kiumbe chema wa Mungu iweje uende
kwenye hizo club kuponda maisha, iweje unywe pombe, iweje ufanye uzinzi na
uasherati badala ya kukaa chuoni ukasoma, iweje ugome kufanya mtihani hadi upate
‘kibuti’?, alihoji huku akishangiliwa na wanavyuo
hao.
Alisema yeye kama mzazi analazimika kuyasema
hayo kwa sababu anatambua kuwa watoto wa leo wamezungukwa na mitego mingi.
“Hatutaki shetani awachezee, ndiyo maana tunawaonya,”
alisisitiza.
Alisema katika kundi kubwa kama hilo wamo
viongozi wa kesho na kwamba wasipojihadhari na kuweka mahusiano yao sawa na
Mungu kuanzia sasa, watajikuta wanafanana na baadhi ya viongozi nchini ambao
wamekabidhiwa dhamana lakini wanakengeuka na kufanya kinyume na matarajio ya
wengi.
Akitoa mfano alisema: “Nchi hii wako wasomi
wengi lakini wamekaa kiwiziwizi tu, fedha za barabara zikitolewa haziendi
kufanya kazi iliyopangwa, wakurugenzi wakipewa fedha za kujenga shule, mabweni
au nyumba za walimu, unakuta zinakamilika lakini ziko chini ya kiwango,
madaktari nao wanaiba dawa za hospitali kwa kutumia magari ya kubebea
wagonjwa.”
“Kama viongozi hawa wangesimama kwenye
nafasi zao (right position) haya mambo yangetoka wapi? Mambo ya mikataba mibovu
yangetoka wapi? Mnadhani nchi hii ingekuwa maskini? Haiwezekani!” alisisitiza
huku akishangiliwa na wanavyuo hao.
Aliwasihi wanavyuo wote watambue nafasi zao
na wazitunze nafasi hizo ili wasimkosee Mungu. “Tunzeni nafasi zenu mlizopewa na
Mungu na wakati wote jitahidini kusikiliza sauti yake, muone jinsi
atakavyowashindia”, alisema.
Mapema, akimkaribisha Mkuu wa Mkoa
kuzungumza na wanafunzi hao, Mchungaji Gerald ole Nguyaine wa Kanisa la ICC –TAG
Dodoma alisema wanafunzi walio katika vyuo hivyo ni wababa na wamama wa kesho
hivyo hawana budi kumtanguliza Mungu katika yote
wayafanyayo.
Naye Mchungaji Gavin Walker kutoka Kanisa la
Calvary Christian Fellowship lililoko Columbus, Ohio, Marekani ambaye alikuwa
mnenaji mkuu katika mkesha huo, aliwasihi wanavyuo kutambua makusudi ya Mungu
ambayo ameyaweka juu yao. “Mungu amekuumba wewe kwa kusudi maalum hivyo ni
lazima ujue hilo kusudi”, alisema.
Alisema kwa kutotambua kusudi la Mungu
katika maisha yao, wako watu ambao wamejikuta wakitaka kufanana na wengine bila
kujua ni kwa nini watu hao wamekuwa hivyo. “Wanatamani nafasi za wengine kwa
sababu tu wao ni maarufu, ni waigizaji, ni wacheza sinema ama wasanii… hapana!
Kila mmoja anatakiwa kujua kusudi ka Mungu katika maisha yake,”
alisisitiza.
Alisema duniani kuna wakazi zaidi ya bilioni
saba lakini wengi kati ya hao wanaishi maisha yasiyotimilika kwa sababu hawamjui
Mungu. “Hakuna kitu ambacho Mungu hawezi kukifanya maishani mwetu, tunachotakiwa
ni kumuomba tu! Kama ni masomo soma kwa bidii huku ukimtumaini Mungu, nawe
utashinda sababu Mungu yuko upande wako,”
alisisitiza.
Aliwaasa wawe wavumilivu wawapo vyuoni.
“Katika maisha ya chuo jifunze kuwa na saburi. Ukijenga saburi sasa hivi tangu
uko chuoni, itakusaidia kuvumilia mengi katika maisha ya mbele baada ya kuhitimu
Chuo Kikuu au chuo chochote unachosoma sasa,” alisisitiza.
Post a Comment