Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Bw. John Nkolo (aliyesimama) akijitambulisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Magesa Mulongo wakati Wajumbe wa Tume hiyo walipokwenda kujitambulisha kwake jana jumapili tarehe 18. Novemba, 2012 tayari ya kuanza kazi ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya katika Mkoa huo. Wajumbe wengine ni Bw. Abubakari Ali, Bw. Ussi Ali na Bi. Mwantumu Malale.
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Bi. Mwantumu Malale akizungumza wakati wajumbe wa Tume hiyo walipokwenda kujitambulisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo jana jumapili tarehe 18. Novemba, 2012 tayari kuanza kazi ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya mkoani humo. Kulia ni Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Magesa Mulongo.
 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mara baada ya wajumbe hao kujitambulisha kwake jana tarehe 18. Novemba, 2012 tayari kuanza kazi ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya mkoani humo. Kutoka kushoto ni Bw. Abubakari Ali, Bw. Ussi Ali, Bi. Mwantumu Malale (na wa kwanza kulia) Bw. John Nkolo.
Na: Ismail  Ngayonga,Arusha. 18. Novemba.  2012
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo ameihakikishia Tume  ya Mabadiliko ya Katiba mazingira mazuri ya utendaji kazi kwa wakati wote wa  kazi ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya Mkoani  humo.
Mkuu huyo wa Mkoa aliyasema hayo (jana jumapili tarehe 18.  Novemba,2012) wakati wa mkutano wake na Wajumbe wa Tume hiyo waliofika Ofisini  kwake kwa ajili ya kujitambulisha tayari kuanza awamu ya nne ya kazi ya  ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya mkoani humo inayoanza leo  jumatatu tarehe 19. Novemba, 2012.
Kwa mujibu wa Mulongo alisema Ofisi yake imejiandaa  kikamilifu kwa ajili ya kazi hiyo na hivyo ipo tayari kutoa msaadakwa Tume hiyo pale inapohitaji. “Katika Mikoa ambayo Tume imeitembelea  kazi hii imepita vizuri na sisi tutahakikisha kuwa sifa hiyo na sisi pia  tunaiendeleza” alisema Mkuu huyo wa Mkoa. 
Aidha Mulongo alisema Tume hiyo imepewa jukumu kubwa la  kitaifa lenye Baraka za Mhe. Rais na Bunge la Jmahuri ya Muungano wa Tanzania,  hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha kuwa anatoa ushirikiano kwa kadri  inavyowezekana.
Kwa upande wake Mjumbe wa Tume hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti  wa kundi la Mkoa wa Arusha, Bi. Mwantumu Malale alisema Tume katika imekuwa  ikitumia njia mbalimbali za kukusanya maoni ya wananchi wakatiwa  mikutano yake ikiwemo njia ya kuzungumza na kuandika.
“Mbali na wananchi pia Viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge  nao wamekuwa wakijitokeza kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya, tunawaomba  wananchi wa mkoa wa Arusha nao pia wajitokeze katika mikutano yetu ili nao  waweze kutoa maoni yao” alisema Bi. Mwantumu.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo jumatatu tarehe 19.  Novemba, 2012 inatarajia kuanza awamu ya nne ya kazi ya ukusanyaji maoni ya  wananchi kuhusu Katiba Mpya katika Mikoa 6 nchini. Mikoa hiyo ni Arusha, Dar es  Salaam, Mara, Simiyu, Geita na Mkoa wa Mji Magharibi,  Zanzibar.
Mkoani Arusha Tume hiyo leo jumatatu inatarajia kuanza  kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya katika Wilaya ya  Karatu.


Post a Comment