|
|

Tangu alipojiuzulu kufuatia tuhuma za kutumia madaraka yake vibaya na
kusababisha taifa kuingia mkataba mbovu ya Richmond, Edward Lowassa, Waziri Mkuu
wa zamani - amebakia kama enigma ndani ya chama chake na kwenye Taifa.
Lakini, vile vile amekuwa ni zaidi ya enigma kwani pia amebakia kama ishara
ya mpiganaji asiyekubali kuweka silaha chini, kurudi nyuma au kusalimu amri.
Lowassa tumeambiwa na tumeshuhudiwa ati kuwa ana "nguvu sana ndani ya chama."
Kwamba mara baada ya kujiuzulu, tulidokezwa kuwa Lowassa alikuwa na nguvu
sana hasa kwa "wenyeviti wa CCM wa mikoa" na hivyo ana mtandao mkubwa sana na
wenye ushawishi (influential) katika ngazi mbalimbali za mikoa.
Pamoja nguvu hiyo kwenye chama tuliambiwa mapema sana mwaka 2008 kuwa Lowassa
alikuwa na nguvu sana kwa wakuu wa wilaya ambao wengi waliteuliwa wakati yeye
akiwa Waziri Mkuu.
Lowassa pamoja na udhaifu wote aliouonesha katika kushughulikia suala la
Richmond bado alikuwa na nguvu sana bungeni.
Kule bungeni tuliambiwa alikuwa na kundi la wabunge ambao waliapa kwake
wakiamini kuwa alionewa sana, hivyo mara moja walisimama nyuma yake na kuwa
tayari kutumika na kutumiwa naye ili kuhakikisha kuwa anajipanga kuja kulipa
kisasi.
Kundi la wabunge hawa ambao nao wengine walikuwa na nguvu ndani ya chama ndio
walikuwa usalama wa Lowassa kushindwa kushughulikiwa na Bunge.
Ni kuwa yeye ndiye aliyeligawa Bunge pia - wale walioamini kuwa ametendewa
vyema na wale ambao waliamini alionewa na Kamati ya Mwakyembe.
Hawa wa kundi la pili wanaamini kabisa kuwa kosa kubwa la sakata la Richmond
lilikuwa linamuangikia Rais Kikwete mwenyewe.
Na hivyo wanaona kuwa Kikwete kushindwa kusimama na Waziri Mkuu wake dhidi ya
mashambulizi ya inayojulikana kama "Kambi ya Sitta" ilikuwa ni udhaifu
mkubwa.
Kama kulikuwa na utata wa nguvu ya "Kundi la Lowassa' utata huu utakuwa
umeondolewa katika sehemu mbili. Kwanza kwenye uchaguzi wa 2010 ambapo baadhi ya
maadui zake waliangushwa kwa kutumia nguvu kubwa sana na wengine
walitetemeshwa.
Kuanguka kwa Selelii kwa mfano ni ishara tu ya nguvu ya kundi hilo. Lakini
zaidi matokeo ya chaguzi za ndani ya chama ambazo zinaelekea kumalizika wiki hii
yanadokeza kuwa kweli Lowassa ana nguvu ambazo anahofiwa kuwa nazo. Kama nguvu
hizi ni zake mwenyewewa au za kivuli chake tunasubiri kuona.
Kwa muda mrefu tulisikia kuwa kuna mpango wa kutaka kumtenganishia Rais
nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa CCM na hivyo chama kiongozwe na mtu mwingine asiye
Rais.
Tetesi hizi inaonekana kutimia kwani kabla tu ya kuanza kwa mkutano mkuu wa
CCM huko Dodoma tetesi hizi zimekuwa kweli ambapo vikaratasi na hoja mbalimbali
zimekuwa zikitolewa dhidi ya "Mwenyekiti wa CCM".
Kwa mara ya kwanza Mwenyekiti wa CCM nafasi ambayo ilikuwa na nguvu sana huko
nyuma inaonekana kuweza kuulizwa, kukataliwa, na kubezwa. Kwa mara ya kwanza
Mwenyekiti wa CCM anashambuliwa na wanachama wa chama chake na tusije kushangaa
kuwa hata kama atashinda ushindi wake unaweza ukawa kwenye usawa wa chini ya
asilimia 60 za wajumbe.
Baadhi ya Mawaziri na wana CCM wengine ambao walijipambanua kuwa wanapiga
vita ufisadi nguvu yao inaonekana haipo. Wameshindwa kusimamia "kujivua gamba"
na wote wameshindwa kutetea CCM dhidi ya ufisadi.
Kama nilivyoondika miezi kadhaa huko nyuma kusema Lowassa asijiuzulu tuone
wana CCM watafamfanya nini na ukweli ni kuwa Lowassa, Chenge, na wanachama
wengine ambao wamehusishwa na vitendo vya ufisadi wamegangamala ndani ya CCM na
hakuna aliyethubutu kuwaondoa.
Chombo pekee bila ya shaka cha kuweza kuwaondoa bila nafasi ya kukata rufaa
ni Mkutano Mkuu wa CCM (ambao unaendelea) na kama huu utashindwa kuchukua hatua
dhidi ya wanachama wake wanaotuhumiwa ufisadi basi tutakuwa na ushahidi mkubwa
tu kuwa CCM siyo sawa na chama cha Kikomunisti cha China.
Kule China kulikuwepo na mwanasiasa mashuhuri sana ambaye kama mambo
yasingegeuka kinyumenyume ndiye alikuwa anaandaliwa kuja kurithi kiti cha Hu
Jintao RAis wa China na Mwenyekiti wa CCP.
Bo Xilai alikuwa ni mwanasiasa aliyeibuka na kupata umaarufu mkubwa kutokana
na siasa zake za mrengo wa kushoto na akipendwa na maelfu ya watu. Lakini sifa
zake zote zimekuja kutoweka mara moja baada ya yeye mwenyewe kuhusishwa na
vitendo vya ufisadi na mke wake kushtakiwa kwa mauaji ya mfanyabiashara wa
Kiingereza.
Hatimaye Bo aliondolewa katika nafasi mbalimbali za chama na wiki chache
zilizopita kabla tu ya Mkutano Mkuu wa CCP (Kama huu wa CCM) Bo alitimuliwa
kutoka kwenye chama na kuna uhakika wa kutosha tu kuwa atashtakiwa kwa makosa ya
kihalifu.
CCM siyo CCP kwani japo wanachama wake kadhaa wa ngazi za juu wameshashtakiwa
na kuhusishwa na ufisadi hakuna hata mmoja aliyevuliwa uanachama!
Kushindwa kwa CCM kujivua gamba kunathibitisha kile kilichosemwa na wengine
gamba limeganda; haliganduki. Na kushindwa huku kunatokana kwa kiasi kikubwa na
kushindwa kwa mifumo ya CCM kwani karibu kila anayetakiwa kumsafisha mwenzie
yeye mwenyewe ni mchafu.
Katika uchangu huu hata Mwenyekiti wa CCM na familia yake hawajaachwa nje na
hivyo kuthibitisha tu hakuna mtu wa kuweza kumsafisha mwingine. Na hapa ndipo
ilipo siri ya nguvu ya Lowassa na kundi lake.
Miezi kadhaa huko nyuma niliwahi kuzungumza na mmoja wa watu wa karibu sana
na Lowassa ambaye aliniambia neno lile lile - kwani nani msafi ndani ya CCM
Mwanakijiji? aliniuliza.
Inawezakana wapo wasafi ndani ya CCM lakini kama wapo hawana nguvu. Nguvu
walizonazo ama zinatokana na nafasi zao na siyo na kanuni walizonao.
Kwa mfano, mtu ambaye ni waziri anaweza kuwa na nguvu kwa kadiri ya kwamba ni
waziri akitoka uwaziri anakuwa kimya. Nje ya madaraka hakuna wana CCM wenye
ujasiri wa kupambana na ufisadi. Hapa ndio crux of the matter ipo.
Ni wana CCM gani wanaweza kusema wanataka chama kisafishike bila ya wao
wenyewe kujiletea matatizo? Wale waliojitokeza kupambana na ufisadi walijikuta
wamewekwa alama ya kushughulikiwa.
Kama kweli Lowassa ana nguvu hiyo ambayo anadaiwa kuwa nayo - wengine
wanasema ana nguvu hadi ndani ya Usalama wa Taifa - basi yumkini ndiye mtu
anayeweza kuja kuwa Rais baadaye. Na atakuja kuwa Rais si kwa sababu ya nguvu
alizonazo bali kwa vile anaogopwa.
Fikiria kuwa badala ya uwepo wa vipeperushi dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi
kuna vipeperushi dhidi ya Mwenyekiti wa CCM! Kama ni hivi basi CCM inabidi
imwachie Lowassa chama na wale wengine watoke maana sioni uwezekano wa hawa
kukaa pamoja.
Kuna njia moja tu ya kumzuia Lowassa na timu yake kuja kushika madaraka ya
Taifa; njia ambapo itahakikisha kuwa CCM inasafishwa kweli kweli.
Njia hii bila ya shaka inahusiana moja kwa moja na wana CCM kuukataa ufisadi,
ahadi za ufisadi, mafao ya ufisadi na utegemezi wa ufisadi. Kwa vile hili ni
gumu kama tulivyoliona inaonekana njia sasa ni nyeupe kwa Lowassa na timu yake
kujikita ndani ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015.
Lakini haya yote yanatufanya tujiulize: Kama Lowassa ambaye alivunja sheria
kadha wa kadha wakati wa suala la Richmond, aliyejiuzulu kwa kashfa na ambaye
hakuwa na nafasi yoyote ndani ya chama ameweza kuwa nguvu kubwa ndani ya CCM
namna hii ina maana CCM ina matatizo makubwa zaidi siyo? Ina maana uadilifu
umegonga mwamba na ufisadi umetamalaki.
Kuna nafasi moja tu iliyobakia kwa CCM kushughulikia ufisadi na mafisadi
ndani ya chama hicho - kupitia Mkutano huu Mkuu. Wakishindwa hawa, na kama
makuwadi wa ufisadi wakipata majukwaa na wakasimama bila kujeruhiwa basi CCM
itakuwa imejiroga yenyewe na Watanzania watakao mabadiliko watashukuru.
Kwa sisi wengine tunaombea CCM iendelee kushindwa kushughulikia ufisadi na
mafisadi kwani hii ndio njia rahisi zaidi ya kukiondoa madarakani. Kushindwa kwa
CCM kujisafisha ni dalili kuwa CCM ya sasa siyo "ile".
Ni kushindwa kwa Mwenyekiti wa CCM (labda ni kweli anatakiwa ang'oke); ni
kushindwa kwa Kamati ya Maadili ya CCM na ni kushindwa kwa wanachama waadilifu
ambao wamebakia kutoa matamko na malalamiko.
Tulivyoona kwenye uchaguzi wa Mwenyekiti na jinsi nguvu kubwa aliyotumia mzee
Makamba kumpigia debe (kumwombea) Rais Kikwete ni wazi kulikuwa na hofu kubwa
sana ya kura za maruhani. Kiasi cha kufikia utaratibu kubadilishwa ili kuweza
kubaini ni mikoa gani itapiga zaidi kura za maruhani hofu ya Lowassa ni kubwa
zaidi.
Tulioangalia upigaji kura imeshangaza kuona kuwa CCM imeshindwa kuendesha
uchaguzi mzuri wa Mwenyekiti na badala yake ilikuwa ni kama kura sokoni. Je
uchaguzi ulikuwa wa haki na huru? Kama Kikwete anakubalika na kupendwa sana na
amefanya mengi kwanini kulikuwa na hofu ya yeye kukataliwa?
Ndio maana naamini hofu ya Lowassa na kundi iko ndani ya CCM tu na mkutano
huu umethibitisha kuwa kweli ana nguvu ndani ya hicho chama japo siyo nguvu
timilifu kama inavyodhaniwa.
Lakini kama kuna watu nje ya CCM wenye kuihofia "nguvu ya Lowassa" na kwamba
wanatetemeka jina lake likitajwa au wanatafuta kupiga magoti mbele zake basi
Lowassa ana nguvu kubwa katika pysche ya taifa.
Chanzo: Tanzania Daima
|
|
on Wednesday, November 14, 2012
Post a Comment