Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Okello Oryem, alisema waasi wanataka malalamiko yao ambayo ni mengi yanayohitaji siku mbili au zaidi ili yajadiliwe na viongozi wa nchi za maziwa makuu, huku kwa sasa viongozi hao wakisema hatua ya vikosi hivyo kuikalia Goma ni kinyume na sheria.
Hata hivyo, msemaji wa M23 amesema viongozi wake bado hawajasema lolote lakini suala la kuondoa vikosi mjini Goma sio kikwazo.
“Hatuelewi nini Uganda walizungumza na viongozi wetu, lakini kile ninachoweza kusema ni kuwa kuondosha vikosi eneo la Goma sio tatizo kubwa. Tunaweza kuviondoa hata sasa, jioni hii au hata muda wowote, ” alisema Amani Kabasha alipokuwa akizungumza na Reuters.
Msemaji wa Serikali ya Congo Lambert Mende alisema hana shaka kuwa serikali ya Uganda imefanya mazungumzo na kiongozi wa waasi Sultan Makenga.
Mende amesema wameambiwa kuwa ombi la kuondosha vikosi vya M23 limekubaliwa, lakini kwa sasa wanasubiri matokeo ya uamuzi huo.
Wakati huo huo, mkuu mpya wa majeshi ya ardhini nchini Congo, Jenerali Francois Olenaga, amesisitiza kwamba wanajiandaa kwa hali yoyote itakayotokea.
“Sichezi mchezo wa adui au marafiki. Sisi ni serikali halali iliyochaguliwa na wananchi wa Congo. Sisi ni jeshi la taifa. Hatuwezi kufuata njia isiyo halali ya M23 au wale wanaowasaidia kutuhujumu.
Wakongo wote wanajua kwamba tumeshambuliwa na tutachukua hatua dhidi ya mashambulizi,” alisema Jenerali Olenaga wakati akizungumza na waandishi wa habari.