MANCHESTER, England
“Nililazimika kumtema tena nje ya kikosi baada ya
kumuona hajafanya kazi ipasavyo kwa takribani siku tatu hivi. Anahitaji kufanya
kazi kwa bidii. Kama mchezaji hafanyi kazi nzuri, hastahili kucheza”
MTALIANO anayeinoa Manchester City, Roberto Mancini – leo
amemtosa nje ya kikosi chake kwa mara pili mfululizo mshambuliaji wake Mario
Balotelli, kutokana na mtazamo hasi anaoonesha mazoezini.
Kocha huyo wa mabingwa wa England, alilazimika kumtupa nje
ya kikosi Balotelli na kumtimua katika hoteli ambayo timu iliweka kambi kuelekea
pambano la Jumapili iliyopita la ushindi wa 2-1 dhidi ya Spurs.
Kuelekea mechi ya jana dhidi ya Aston Villa, Mancini
alisisitiza kwa kumtaka nyota huyo kuimarisha kiwango chake na utayari wake
mazoezini, ikiwa anahitaji hasa kuvaa tena jezi ya Manchester City.
Mancini alisema mapema jana kuwa: “Nilimwambia baada ya
mazoezi ya leo Jumamosi asubuhi kuwa, hatokuwa sehemu ya kikosi changu cha mechi
ya mchana.
“Nililazimika kuchukua uamuzi huo baada ya kumuona
hajafanya kazi ipasavyo kwa takribani siku tatu hivi na binafsi sipendi hilo
jambo.
“Ni juu ya mtazamo wake mazoezini, nazungumzia kuhusu hilo.
Anahitaji kufanya kazi kwa bidii. Kama mchezaji hafanyi kazi nzuri, hastahili
kucheza.
“Unachokifanya mazoezini, ndicho utakachofanya dimbani
wakati wa mechi. Hivyo kila mchezaji anapaswa kufanya kazi kwa bidii mazoezini
na kuboresha kiwango chake.”
Post a Comment