Ndugu Zangu,
Katika maisha kuna wanaogopa kushindwa. Njia nyepesi ya kuepuka kushindwa ni kutoshindana. Kwa mwanadamu, hapo utakuwa umeshashindwa kabla ya kushindana.
Na siku zote, mshindi mzuri ni yule aliyeshindwa mara nyingi. Barack Obama ni mfano wa mshindi mzuri, maishani mwake Obama ameshindwa mara nyingi, ni kwenye familia na siasa pia.
Hakika, si wengi wenye kutambua, kuwa Barack Obama ni mfano wa wanasiasa walioshindwa mara nyingi, lakini, kamwe hakukata tamaa. Kuna mifano kadhaa ya kushindwa kwa Obama kwenye njia yake ya kuelekea kwenye kushinda tuzo ya juu kabisa Mmarekani anaweza kuishinda; Urais wa Marekani.
Na sasa, Barack Obama ameshinda mara mbili kwenye kuiwania tuzo hiyo. Na hiyo mara ya pili ina maana kubwa mno kwa Obama. Maana, angeshindwa mara hiyo, Barack Obama asingekuwa tena na nafasi ya kuishindania tuzo hiyo.
Nimesoma maandiko kadhaa yenye kuelezea njia ya Obama kuelekea kwenye kushinda tuzo hiyo ya juu kabisa, moja ya anguko la Obama njiani ni pale, kama wasemavyo Waswahili, ‘alipogalagazwa’ na Mmarekani mweusi, Mzee Bobby Rush, ni mwaka 2000, kwenye Uchaguzi wa kuingia kwenye Baraza la Halmashauri kule Chicago. Obama , akiwa kijana na msomi wa Chuo Kikuu alipambana na mzoefu wa siasa, Mzee Rush, na kilichomtokea ni kuambulia kura chache.
Obama hakuwa mzoefu kwenye mijadala. Aliongea kisomi zaidi, na hadhira yake haikumwelewa. Wakati Mzee Rush alikuwa mzoefu wa siasa, na aliongea lugha ya watu na alilimudu sana jukwaa.
Obama alipotakiwa kutoa maoni yake baada ya anguko lile alitamka; “ Kwangu kilichonitokea ni kama kupata ‘Elimu ya Siasa’!”
Ni hapo, ndipo Obama alipoanza kujifunza zaidi misingi ya kushindwa, kusimama, na kuendelea kupambana, na hatimaye kushinda, na zaidi, kujifunza kutokana na kushindwa.
Naam, siku zote, panapo ushindani kuna kushinda na kushindwa. Busara ni kujitayarisha na kushinda au kushindwa.
Na hilo ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
Post a Comment