Picha ya shilole na makala enzi hizo |
TAARIFA
mbalimbali zilizowahi kutolewa na mwigizaji na mwanamuziki maarufu nchini,
Zuwena Mohamed 'Shilole' kuhusu uhalisia wa maisha yake zimeelezwa kuwa si za
kweli, kwa mujibu wa watu wa karibu na staa huyo.
Shilole aliwahi kuliambia Mwanaspoti Toleo la Septemba 22
mwaka huu lililofanya naye mahojiano kuwa mtoto wake wa kwanza mwenye umri wa
miaka 10 alijifungua baada ya kubakwa na baba wa mtoto huyo ambaye amedai kuwa
wawili hao walishaishi kama mke na mume kwenye nyumba ya familia ya mume huko
Igunga, Tabora.
"Shilole nilijuana naye tangu mwaka 2000, kwa wakati huo
alikuwa amemaliza darasa la saba.
Ukweli ni kwamba wote tulikuwa watoto, mwenzangu hakuwa na
uangalizi wa karibu na familia yake kwani alikuwa hana wazazi nami pia nilikuwa
sina wazazi bali nilikuwa na dada mmoja tu, tulianza kuishi pamoja katika nyumba
ya familia," anaanza kwa kusema Makala Joseph mwanamume aliyezaa na Shilole
mtoto wa kwanza.
Anasema licha ya kwamba alimkana, akamkimbia, akamsusia
mtoto na baadaye akaja kumwiba kwa siri, lakini bado anampenda na kumsihi kama
atarudisha moyo wake yupo tayari kumpokea kama mkewe, kwani bado hajaoa
akimsubiri Shilole.
Makala ambaye sasa anaishi Igunga mkoani Tabora akifanya
kazi ya utingo, anasema kauli ya staa huyo ina athari kubwa kwa mtoto ambaye
sasa bado ni mdogo.
"Unaposema kuwa ulibakwa haileti picha na mtazamo mzuri kwa
watu, hata hivyo kwa mtoto pia ina athari kubwa, anakua na itafikia kipindi
atataka kujua ukweli wa maisha ya mama yake, atakaposikia mama yake alibakwa
italeta picha gani?
"Tulikubaliana mpaka tukaishi miaka miwili na kuzaa mtoto
ambaye mwenzangu alikimbia na kuniachia mtoto akiwa na miezi mitano mara baada
ya kukutana na dereva wa magari makubwa na si kwamba nilimbaka, kama ni hivyo
kwanini asingeenda mahakamani na kufungua kesi?" Alihoji
Makala.
Anasema ingawa anamtunzia mtoto wake, si vema kwa Shilole
kuzungumza kauli zisizo za kweli na kuficha ukweli, huku akiwapakazia watu
wengine kesi zisizo kweli.
"Leo ananiona mimi mshamba. Sawa lakini akumbuke kuwa
alitoka huku ni vema kuheshimu sehemu uliyotoka kuliko kuleta
dharau.
Mimi si msemaji ila tu nimechoshwa na kauli zake, kila siku
kwenye magazeti eti alibakwa huku mtuhumiwa nipo kwanini asingeshtaki, hakuna
asiyejua hapa Igunga kama niliishi naye kama mke wangu.
"Wakati huo mimi nilikuwa utingo na yeye alikuwa akiuza
nyanya sokoni.
Maisha yaliendelea hivyo mpaka alipokuja kupata ujauzito na
baadaye alijifungua.
Ila nyongo ilitumbukia baada ya yeye kukutana na huyo bwana
ambaye alimshawishi akimbie kwangu na akaenda kumzalisha huko Dar es
Salaam."
Kauli ya Makala inafafanuliwa zaidi na dada yake Sara Joseph
ambaye ndiye wifi wa Shilole: "Ni kweli yeye hana wazazi kama anavyoeleza katika
mahojiano yake kwenye magazeti, redioni na runinga.
Lakini kuna baadhi ya mambo anayoyasema si ya kweli.
Angezungumzia maisha yake halisi mimi sina neno, adanganye anavyotaka, lakini si
hilo la kuhusu mtoto.
"Kila mtu anajua ipo siku mtoto atakuwa katika hali mbaya na
atakuja kutulaumu sisi, kama ameshindwa kulea mtoto atuletee na si kusema
alibakwa haileti picha nzuri kwa familia yetu."
Sara ambaye sasa anaishi jijini Dar es Salaam anaeleza namna
alivyoilea familia hiyo wakati akiishi Igunga.
"Nilimpokea Shilole akiwa mdogo sana, wakati huo alikuwa
akiishi kwa bibi Tatu ambaye ni ndugu wa mama yake aliyeishi na kaka zake
wengine wawili Kajiwe na Pascal.
Alikuja na kuanza kuishi na mdogo wangu, kwa kuwa nilikuwa
mkubwa nilichukua jukumu la kuwalea wote.
Hii ina maana kuwa hajawahi kusoma sekondari kama anavyodai
bali alizaa na mdogo wangu baada ya kuishi naye kwa miaka
miwili.
"Ugomvi ulianza kwa kuwa Shilole alikuwa anapenda starehe
kuliko mtoto, alitaka kumwacha mtoto na kumfuata mumewe kwenye starehe wakawa
wanabishana kila siku mpaka alipokutana na dereva wa magari makubwa akatoroka na
kuniachia mtoto akiwa na miezi mitano.
Niliitwa na mtu na kuambiwa kamchukue shangazi yako kajinyea
ndipo nilipomkuta mtoto ametelekezwa na yeye amekimbia na bwana," anasema
Sara.
Anasema Shilole alirudi Igunga wakati mtoto wake akiwa na
umri wa miaka sita. "Nilimlea mtoto mpaka alipotimiza miaka sita, alirudi Igunga
na kumchukua mpaka mwaka jana alipomleta kunisalimia wakati wa likizo akiwa na
miaka tisa," anasema.
Hata hivyo, wifi wa Shilole anasema baada ya kumpigia
akimtaka ajibu tuhuma za kubakwa alijibu: "Nimeandika habari zangu za maisha
yangu." Kauli iliyozidi kumfanya ahisi itamharibu mtoto atakapokuwa
mkubwa.
Mwanaspoti lilipomtafuta Shilole atoe kauli yake kuhusu
suala hilo alisema: "Sina la kujibu kuhusu hilo kwa kweli na kwa sasa nipo bize
sana kwani nipo katika matayarisho ya filamu mpya hapa."
SOURCE:http://mwanaspoti.co.tz/
Post a Comment