Gavana wa Jimbo la Kivu
ya Kaskazini amesema, kuwa waasi wa M23 hawana uwezo wa kuuteka mji wa Goma,
Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kufuatia mapigano
makali.
Julien Paluku amesema
wapiganaji hao wa waasi walikuwa wamempigia simu kumjulisha kuwa watawasili leo
usiku mjini Goma.
Paluku amesema wanajeshi
150 wa waasi wameuawa lakini msemaji wa waasi hao amekanusha habari
hizo.
Mapigano hayo ndiyo
mabaya zaidi tangu mwezi Julai mwaka huu katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa
wa madini.
Zaidi ya watu laki tano
wamehama makwao tangu mwezi Aprili mwaka huu, wakati wanajeshi kadhaa walipoasi
kutoka kwa jeshi la Serikali.
Mapigano hayo yamekuwa
yakiendelea karibu na kijiji cha Kibumba takriban kilomita 30 Kaskazini mwa
Goma.
Gavana wa Jimbo la Kivu
ya Kaskazini Julien Paluku ameiambia BBC kuwa mapigano hayo yanaendelea hadi leo
siku ya Ijumaa.
Umoja wa Mataifa
unazishtumu Rwanda na Uganda kwa kuwaunga mkono waasi, shutuma ambazo zinapingwa
na nchi zote mbili.
Mwandishi wa BBC,
Gabriel Gatehouse amesema kuzunguka kijiji cha Kibumba kiasi cha kilomita 30
Kaskazini mwa Goma hali imekuwa mbaya zaidi tangu mwezi Julai.
Amesema serikali
imepeleka vikosi zaidi, katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na helikopta za
kijeshi, pia askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wameonekana katika
maeneo ya kijiji cha Kibumba.
Pande zote mbili
wamelaumiana kwa kuanzisha mapigano hayo yaliyoanza mapema asubuhi
Alhamisi.
Mwandishi wa BBC amesema
wakati alipokuwa katika eneo linalodhibitiwa na waasi Jumatano, aliwaona waasi
wa M23 ambao pia hujulikana kama Jeshi la Ukombozi la Congo wakisambaza askari
wake na kujiandaa kwa vita.
Watu wanakimbilia
kuelekea Kusini ambako majeshi ya serikali yanadhibiti maeneo hayo wakiwa
wamebeba mizigo yao vichwani.
Baadhi yao wamekuwa
wakienda katika kambi kubwa ya Kibai iliyopo katika vitongoji vya kaskazini mwa
Goma.
Msema wa Umoja wa
Mataifanchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Luteni Kanali Prosper Basse,
amesema pia kumekuwa na mapigano kilomita 90 kaskazini mwa Goma, huku majeshi ya
serikali yakitwaa mji wa Mabenga na kusonga mbele kuelekea mji wa Kiwanja ambao
ni mji muhimu wa waasi.
Post a Comment