Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

SERIKALI YAFUTA LESENI YA KAMPUNI YA UCHIMBAJI DHAHABU

Serikali imefuta leseni za uchimbaji kwa Kampuni ya Uchimbaji wa Dhahabu ya Aureus Limited iliyopo jijini Mwanza, baada ya kubainika kuficha taarifa za mauzo ya madini hayo na kuikosesha mapato yenye thamani ya Sh. bilioni 10.7.

Aidha, Mmiliki wa kampuni hiyo ambaye anaishi Barcelona nchini Hispania, Marc Rene Roelandts, aliyekuwa anasakwa na serikali kwa tuhuma hizo amekamatwa na kurejeshwa nchini ili kujibu mashtaka yanayomkabili.

Akizungumza na NIPASHE mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, aalisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.

“Jalada lipo kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), hawa wote watatu watapelekwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa baada ya DPP kutoa kibali cha kushtakiwa kwa watu hao,” alisema.

Aliwataja wanaotarajiwa kufikishwa makamani wakati wowote kuwa ni raia wa Uholanzi ambaye ni kiongozi wa shughuli zote za kampuni hiyo, David Gommeren (43); raia Afrika Kusini ambaye ni Mkuu wa Uzalishaji wa Kampuni hiyo, Gidion Ludwick) na raia wa Israel, Andrey Vash (44).

Septemba mwaka huu, Masele alisema Roelandts anamiliki hisa moja na Kampuni ya MS Quaester Limited ya Mauritius inayomiliki hisa 999.

Alisema kampuni hiyo inamiliki mitambo miwili ya uchenjuaji ambayo ipo katika kijiji cha Nyarugusu wilayani Geita na mtambo wa pili upo Nyakato jijini Mwanza.

Masele alisema Agosti hadi Septemba mwaka jana, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA) ulifanya ukaguzi wa hesabu za fedha kwa kampuni hiyo ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama Minextech ambayo ni Kampuni ya uchenjuaji wa marudio ya dhahabu kwa wachimbaji wadogo kwa kutumia teknolojia ya Kemikali ya Sayanaidi.

“Ukaguzi huo uligundua kasoro kadhaa zilizoikosesha serikali mapato ikiwamo Kampuni ya Minextech kuficha taarifa zake za mauzo ya dhahabu kiasi cha kilo 63.27 yenye thamani ya Sh. 2,763,426,787 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi 2010,” alisema.


Alisema udanganyifu huo ulibainika baada ya kulinganisha na taarifa za mauzo ya dhahabu zilizowasilishwa serikali na kampuni hiyo katika kipindi husika.

“Kampuni ya Minetech kutolipa kiasi cha Shilingi 9,085,031,656 kama VAT (Kodi ya ongezeko la thamani), ya mauzo ya dhahabu katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2010.”

Alisema pia kampuni hiyo ilibainika kutolipa Sh. 252,683,678 kama kodi ya mishahara (Paye) katika kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi 2010.

Aidha, kampuni hiyo ilibainika kutolipa mrabaha wa Sh. 371,026,716 katika kipindi cha kati ya mwaka 2006 hadi 2010.

Masele alisema hatua stahiki zinaendelea kuchukuliwa na serikali ili kuhakikisha malipo hayo yanafanyika.

“Serikali imechukua hatau za awali za kuhakikisha kuwa wahusika wote wanakamatwa na kufunguliwa mashitaka. Tayari viongozi wakuu wa kampuni hiyo wapo mikononi mwa Jeshi la Polisi na uchunguzi zaidi unaendelea kabla ya serikali kuchukua hatua zinazostahili,” alisema na kuongeza:

“Tukio hili linadhihirisha wazi kuwa Kampuni ya Aureus Limited ilikuwa imekusudia kuficha kiasi halisi cha uzalishaji wake kwa lengo la ukwepa kulipa mrahaba na kodi stahiki.”

Alisema hatua zitakazochukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufutiwa leseni na kutaifishwa kwa mgodi huo.

Aliongeza kuwa serikali imejipanga vizuri kubaini na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaojihusisha na udanganyifu katika shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchini.

“Wote watakaopatikana kutenda kosa hilo watachukuliwa hatua kazi za kisheria ikiwa pamoja na kufutiwa leseni zao na kuzuiliwa kujishughulisha na shughuli za madini hapa nchini,” alisema.

Aidha, alisema wawekezaji hao walikuwa wakituhumiwa kuwadharau viongozi wa serikali, kutoa lugha za matusi kwa nyakati tofauti ikiwamo wakati Waziri wa Mambo ya Mambo ya Ndani ya Nchi (sasa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Shamsi Vuai Nahodha, alipoutembelea mgodi huo.

Kadhalika, wawekezaji hao wanadaiwa kwa makusudi kukiuka makubaliano kati yake na serikali yaliyofikiwa kwa lengo la kudhibiti shughuli zake za uzalishaji.

Alisema Septemba 9 mwaka huu, kwa kuwadanganya wakaguzi kuwa wasingefanya uzalishaji wa dhahabu siku hiyo na badala yake wangefanya Septemba 10, mwaka huu.

Hata hivyo, wakaguzi hao waligundua kuwa kulifanyika uzalishaji Septemba 9, mwaka huu baada ya kuambiwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya wabunge kulalamikia kampuni hiyo kutorosha nje madini hayo.

Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed, aliwahi kulieleza Bunge kuwa kampuni hiyo imekuwa ikizalisha wastani wa kilo 15 kwa wiki na kuzitorosha nje ya nchi bila kulipa kodi kwa serikali.

Masele alisema kufuatia tuhuma hiyo, Wizara kupitia TMAA ilichukua hatua za haraka kwa kuweka usimamizi makini wa shughuli za uzalishaji za kampuni hiyo ili kubaini ukweli.

CHANZO: NIPASHE
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top