Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Serikali yakwama kwa Muro, warudi kujipanga


Jerry Muro
                                                   **************
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeiruhusu Jamhuri kufanya marekebisho katika hati ya sababu za rufaa ya kupinga hukumu iliyomuweka huru aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), Jerry Muro na wenzake wawili, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya rushwa.

Mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo jana baada ya mrufani (Jamhuri) aliyekuwa akiwakilishwa na jopo la mawakili watatu wa Serikali kuomba kufanya marekebisho katika rufaa hiyo, wakati rufaa hiyo ilipotajwa.

Baada ya kuridhia maombi hayo, Jaji Dk Fauz Twaib anayesikiliza rufaa hiyo alimpa mrufani huyo siku moja kuwasilishwa mahakamani hati ya sababu za rufaa iliyofanyiwa marebisho. Hivyo aliamuru rufaa hiyo iliyofanyiwa marekebisho iwasilishwe mahakamani hapo leo. Jaji Dk Twaib alipanga kusikiliza rufaa hiyo Februari 12 mwaka 2013, ambapo mahakama itasikiliza hoja za pande zote, kabla ya mahakama kutoa hukumu yake.

Katika usikilizwaji huo mrufani atatoa hoja zake za kupinga hukumu hiyo ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyowaweka huru Muro na wenzake, na upande wa wajibu rufaa kujibu hoja hizo. Muro na wenzake, Edmund Kapama maarufu kama ‘Dokta’ na Deogratius Mugassa, walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama na kuomba rushwa ya Sh10 milioni, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hata hivyo Novemba 30, 2011, mahakama hiyo,katika hukumu iliyotolewa na Hakimu Mkazi, Frank Moshi aliyekuwa akiiskiliza kesi hiyo, aliwaachia huru washtakiwa hao.

Hakimu Mosha alisema kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao na kwamba pingu, bastola, risiti na miwani ambavyo alikutwa navyo Muro, havikutosheleza kuonyesha ni jinsi gani vilishiriki katika makosa hayo.Vifaa hivyo viliwasilishwa mahakamani na upande wa mashtaka kama vielelezo vya ushahidi katika kesi hiyo.

Pia Hakimu Moshi, katika hukumu hiyo alieleza kushangazwa na Wage ambaye pia alikuwa mmoja wa mashahidi wa upande wa mashtaka, kwa kushindwa kutumia nafasi yake akiwa mtumishi wa Serikali, kuwaomba watuhumiwa hao kumwonyesha vitambulisho walipojitambulisha kuwa wao ni maofisa kutoka Takukuru.

Hata hivyo upande wa Mashtaka (Jamhuri) ulidai kuwa haukuridhika na hukumu hiyo na siku hiyohiyo uliwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa, na baadaye Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alikata rufaa Mahakama Kuu kupinga hukumu hiyo ya Mahakama ya Kisutu.

Muro na wenzake walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Februari 5, mwaka 2010, na kusomewa mashtaka kula njama na kuomba rushwa kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage.

Akiwasomea mashtaka hayo aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi katika ofisi ya (DPP), Stanslaus Boniface (marehemu), alidai kuwa katika shtaka la kwanza kuwa washtakiwa walikula njama na kinyume cha kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa, ya mwaka 2007.

Katika shtaka la pili alidai kuwa Januari 29, mwaka 2010, washtakiwa waliomba rushwa ya Sh10 milioni, kutoka kwa Wage, kinyume cha kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.

Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo katika Hoteli ya Sea Cliff Dar es Salaam, ili wasitangaze kwenye televisheni habari za tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma ziklizokuwa zikimkabili Wage akiwa mhasibu wa halmashauri hiyo.

Shitaka la tatu lilikuwa likiwakabili mshitakiwa wa pili, Kapama ‘Dokta’ na mshitakiwa wa tatu, Mugassa.

Alidai kuwa washtakiwa walijitambulisha kuwa ni maofisa wa Takukuru kinyume cha kifungu cha 100 B cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, kikisomwa pamoja na kifungu cha 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya mwaka 2002.


Chanzo: Mwananchi
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top