Wasimamizi wa uchaguzi nchiniSierra Leonewamesema uchaguzi mkuu nchini humo umefanyika kwa amani na uwazi na kwamba watu wengi walijitokeza jana kupiga kura, ingawa baadhi ya vituo vya kupigia kura vilichelewa kufunguliwa.
Hamid Goutierez, msemaji wa kituo cha waangalizi cha Carter, amesema katika suala la taratibu kwa ujumla wamebaini ni mchakato unaoaminika. Mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya, Richard Howitt amesema wananchi wengi wa Sierra Leone wamesema uchaguzi wa mafanikio utakuwa ishara ya nchi hiyo kusonga mbele kutoka kwenye taifa linalojitoa kutoka mzozo wa vita na kuwa taifa la maendeleo.
Huu ni uchaguzi wa tatu kufanyika tanguSierra Leoneitoke kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2002, ambapo watu 50,000 waliuawa. Rais aliyeko madarakani, Ernest Koroma na chama chake tawala cha All People’s Congress anapambana na Julius Maada Bio, kiongozi wa zamani wa kijeshi.
Matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kutangazwa ndani ya siku kumi.